Na Asha Kigundula
KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa, Taifa Stars Kim Poulsen, amesema mchezo wake wa Jumamosi dhidi ya timu ya Taifa ya Malawi ndiyo utakaompa sura ya kikosi chake kipya.
Mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa utafanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kabla ya Taifa Stars kuvaana na Ivory Coast katika mchezo wa kufuzu kwa Kombe la Dunia 2014.
![]() |
Kocha wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' Kim Poulsen. |
Alisema anaamini kila mchezaji aliyemuita ana uwezo, lakini ni nani watakuwa kwenye kikosi kitakachoivaa Ivory Coast, hicho ndiyo kitapatikana mara baada ya mchezo huo.
"Ni kweli kila niliyemuita nina imani naye kuwa anaweza, lakini nani na nani watakakuwepo kwenye kikosi changu vja Ivory Coast nitajua mara baada ya mchezo wa wiki hii na Malawi," alisema.
Poulsen, alisema wachezaji wake wana ari kubwa ya mazoezi na anaamini kila kitu kinawezekana katika mchezo wake ujao.
Stars itajitupa na timu ya taifa ya Malawi (The Flames) katika mchezo wa kirafiki wa kujipima nguvu kabla ya kwenda mjini Abijan kuvaana na Ivory Coast Juni 2 mwaka huu.
Wakati huo huo, kikosi cha timu ya Malawi kinawasili nchini leo kwa ajili ya mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa.
Baadaye, Malawi itakwenda Zanzibar kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Zanzibar Heroes, itakayofanyika Mei 28 mwaka huu, kabla ya kuondoka Mei 30 kwenda Uganda, ambapo Juni 2, nao watacheza mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia Kanda ya Afrika na The Cranes.
No comments:
Post a Comment