- MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Wednesday, May 23, 2012

NMB, SBL waipa Twiga Stars mil 30/-
- Kuagwa leo, watakiwa kuifumua Ethiopia
Na Asha Kigundula
BENKI ya NMB na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) zimetoa sh. milioni 30 kwa timu ya taifa ya wanawake (Twiga Stars) inayotarajia kuondoka nchini leo jioni kwenda Ethiopia kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo.
Twiga Stars inakwenda kwenye mechi ya mchujo ya fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Ethiopia. Mechi hiyo itachezwa Mei 27 mwaka huu.

Kikosi cha timu ya taifa ya Wanawake 'Twiga Stars'.
 Akizungumza Dar es Salaam katika hafla maalum ya kukabidhi hundi hiyo jana, Meneja Masoko wa NMB, Imani Kajuna, alisema wametoa mchango huo kuisadia Twiga kutokana na ushirikiano na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), na bidii inayooneshwa na timu hiyo katika michuano ya Kimataifa.
Kajuna alisema kuwa licha ya kutoa fedha hizo, pia wametoa vifaa vya mazoezi na mechi vyenye thamani ya sh.milioni 5.5. Vifaa hivyo vitawasaidia katika mazoezi na mechi ambazo watacheza nyumbani na ugenini.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Michezo ya Baraza la Michezo la MTaifa (BMT), Juliana Yasoda, amewashukuru kwa kusaidia timu hiyo.
Alisema mchango wao ni mkubwa kwa timu hiyo ambayo bado inahitaji msaada kwa ajili ya kufanikisha mchezo wa soka ya wanawake na mechi hiyo ya Jumapili.
Akitoa shukrani zake kwa niaba ya timu hiyo Kocha Msaidizi wa Twiga Stars, Nasra Mohamed, alisema wameshukuru kwa kupewa msaada huo.
Mohamed alisema kupewa kwao msaada ni kutokana na kukubali ushirikiano wao katika mashindano hayo, nao hawatawaangusha.
Mohamed alisema juzi Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo aliwatembelea kambini na kutoa mshango mkubwa ambao ulilipa posho za siku 19 kwa wachezaji na benchi lake zima la ufundi.

Twiga Stars, wakishangilia katika moja ya michezo yao.
 Twiga inayoondoka leo saa 12 jioni, itaagwa saa 5, asubuhi kwenye Ukumbi wa TFF, ikiwa ni pamoja na kukabidhiwa bendera ya Taifa.
Msafara wa Twiga Stars utakuwa na watu 25 wakiwemo wachezaji, benchi la ufundi na viongozi. Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Lina Kessy ndiye atakayeongoza msafara huo.
Twiga Stars itarejea nyumbani Mei 28 mwaka huu kusubiri mechi ya marudiano itakayochezwa Juni 16 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mshindi ndiye atakayepata tiketi ya kucheza Fainali za Nane za AWC zitakazochezwa Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.

No comments:

Post a Comment