MKANDARASI AELEZA CHANGAMOTO UJENZI SOKO TANDALE - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Friday, January 20, 2023

MKANDARASI AELEZA CHANGAMOTO UJENZI SOKO TANDALE

  Na Mwandishi Wetu

 MKANDARASI Kampuni ya NAMIS Corporate Ltd anayejenga soko la Tandale ameelezea changamoto za kutokamilika kwa wakati kwa soko hilo ikiwemo kutokulipwa kwa wakati.

Msimamizi wa mradi huo, James Msumari, alisema jana kuwa walianza mradi huo Septemba 14, mwaka 2019 bila kupata malipo ya awali kwa ajili ya ujenzi huo na badala yake zililipwa miezi 10 baada ya ujenzi wa soko hilo kuanza. Aliongezea kusema kuwa hali hiyo ya ucheleweshwaji wa malipo uliendelea pia kwa malipo yaliyofuata ambapo ucheleweshwaji ulikuwa kati ya miezi 3 hadi 7.

 Alisema baada ya kuanza kwa ujenzi huo walikutana pia na changamoto kadha wa kadha ikiwemo maongezeko ya kazi ambazo hazikuwa kwenye mkataba wa ujenzi huo.

 Alitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni kulazimika kujenga soko la dharura kwaajili ya kuwahamisha wafanyabiashara walikuwa kwenye soko hilo ili kuwezesha ujenzi kuanza kwa wakati.

 “Tulilazimika kujenga soko la dharura jambo ambalo halikuwemo kwenye mkataba ili tuweze kuwahamisha wafanyabaishara kwaajili ya kuanza ujenzi. Tulifanikiwa kuwahamisha tukaanza ujenzi lakini gharama hizo hazikuwa kwenye mkataba wetu,” alisema

 Msumari alisema ufinyu wa eneo la ujenzi nao umechangia kwa kiwango kikubwa kuchelewa kukamilika kwa mradi huo kwani wanalazimika kuweka vifaa vingi vya ujenzi nje ya eneo hilo.

 “Lile eneo ni finyu sana na wakati mwingine unaleta mzigo mkubwa unauweka mbali na site kisha unaupeleka kidogo kidogo. Na hata ujenzi tunalazimika kuufanya kwa awamu ili kuhifadhi baadhi ya malighafi kwenye eneo hilo,” alisema

 Alisema wanalazimika kuchanganya zege la ujenzi sehemu nyingine na kisha kulisafirisha kwenda eneo hilo kutokana na ufinyu wa nafasi kwenye eneo la ujenzi.

 Alisema ujenzi huo umefikia asilimia 80 na kwamba ingawa Manispaa iliwataka wakabidhi Novemba 2022 waliomba wakabidhi Juni mwaka huu ambapo wanauhakika watakamilisha ujenzi wa soko hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla alitembelea soko hilo juzi kuangalia maendeleo ya ujenzi wake na kumtaka mkandarasi huyo kuongeza kasi ya ujenzi.

Makalla alisema tayari serikali ilishamlipa mkandarasi huyo shilingi bilioni saba kati ya 10 anazodai hivyo alimtaka aongeze idadi ya mafundi ili kukamilisha haraka mradi huo.

“Nyinyi ni kampuni kubwa sana na mmeshalipwa shilingi bilioni saba kati ya shilingi bilioni 10, soko lilipaswa kukamilika mwaka 2020 lakini mmeomba kuongezewa muda wa mkataba mpaka Juni mwaka huu, sasa nawaagiza muongeze mafundi na kazi zifanyike kila siku ili soko likamilike, “ aliagiza Makalla

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, katikati akikagua soko la Tandale juzi kulia ni msimamizi wa mradi huo kutoka Kampuni inayojenga soko hilo ya NAMIS Corporate Ltd, James Msumari.


Mwonekano wa nje wa soko la Tandale linalojengwa na Kampuni ya NAMIS Corporate Ltd.


No comments:

Post a Comment