![]() |
Mtandao wa Polisi Wanawake (TPF NET) Wilaya ya Ruangwa umetoa elimu kwa mama wajawazito na wahudumu wa afya katika wodi ya wazazi ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Zoezi hilo limefanyika Machi 5, 2026 na kuhusisha askari wa kike kutoka Jeshi la Polisi Ruangwa pamoja na majeshi mengine wakiongozwa na Inspekta Vivian Mauya, ambapo wamewakumbusha mama wajawazito umuhimu wa kuzingatia malezi bora ya mtoto ili kujenga kizazi bora kwa taifa la kesho.
Katika elimu hiyo, wanawake pia wamehamasishwa kushirikiana na Jeshi la Polisi katika mapambano dhidi ya uhalifu kwa kutoa taarifa za matukio ya kihalifu yanapotokea katika jamii.
Aidha, askari hao wametoa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia na madhara yake, huku wakisisitiza umuhimu wa haki na usawa kwa wanawake na wasichana katika jamii.
Sambamba na hilo, wanawake wamehamasishwa kuwajibika katika malezi bora ya watoto pamoja na kusimamia maadili mema ndani ya familia.
Akizungumza katika zoezi hilo, Inspekta Vivian Mauya amewahimiza wanawake kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ngazi ya Wilaya na Mkoa, akisisitiza kuwa wanawake wana uwezo mkubwa wa kufanya mambo makubwa zaidi kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.







No comments:
Post a Comment