![]() |
Matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yamefikia asilimia 28.6 mwaka 2025, hatua inayotajwa kuwa ishara ya mafanikio ya juhudi za serikali katika kuhamasisha wananchi kutumia nishati salama na rafiki kwa mazingira.
Hayo yameelezwa Mei 8, 2026 jijini Arusha na Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Nolasco Mlay, wakati wa uzinduzi wa mitungi ya LPG ya LOTI GAS.
Mlay amesema ongezeko hilo linaonyesha kuwa lengo la Serikali la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034 litafikiwa kama ilivyopangwa.
Amesema Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia kwa vitendo kwa kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo ili kuboresha afya za wananchi na kulinda mazingira.
“Matokeo haya yanatia moyo na yanaonyesha dhamira ya Serikali kuhakikisha wananchi wanatumia nishati iliyo salama na yenye manufaa kwa afya na mazingira,” amesema Mlay.
Ameongeza kuwa uzinduzi wa LOTI GAS unaunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa kinara wa kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini na Afrika kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Loti Gas Tanzania, Collins, amesema kampuni hiyo imeamua kuleta mitungi ya gesi yenye gharama nafuu ili kuwasaidia Watanzania wengi kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi.
Amesema bado familia nyingi hutegemea kuni, mkaa na mafuta ya taa kwa ajili ya kupikia, hali inayochangia magonjwa ya mfumo wa hewa pamoja na uharibifu wa mazingira.
“Tunaamini LOTI GAS itakuwa sehemu ya suluhisho la changamoto hizi kwa kutoa huduma nafuu na salama kwa wananchi,” amesema Collins.
Katika hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Arusha , aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla.





No comments:
Post a Comment