NA MWANDISHI WETU, LINDI
MKURUGENZI wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Nolasco Mlay, ametembelea Mradi wa Haidrojeni ya Kijani (Green Hydrogen) unaotekelezwa na Taasisi ya Bora Women Go Green wilayani Kilwa, mkoani Lindi, kwa lengo la kutathmini hatua za utekelezaji wa mradi huo na matumizi ya teknolojia hiyo katika uzalishaji wa nishati safi ya kupikia.
Katika ziara hiyo, Mlay alipokea maelezo kuhusu teknolojia inayotumika katika mradi huo, hatua zilizofikiwa pamoja na maandalizi yanayoendelea kuelekea kuanza kwa uzalishaji rasmi.
Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo, Mlay amesema Serikali inaendelea kuunga mkono na kuhamasisha ubunifu na matumizi ya teknolojia mbalimbali zinazoweza kuongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia nchini.
“Serikali inatambua umuhimu wa teknolojia na ubunifu katika kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia. Ni muhimu kuendelea kuangalia teknolojia mbalimbali, kutathmini ufanisi na usalama wake, pamoja na namna zinavyoweza kufikika kwa wananchi kwa gharama nafuu na kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira,” amesema.
Mradi huo unatumia maji kama malighafi katika mchakato wa uzalishaji wa Haidrojeni ya Kijani kwa ajili ya matumizi ya kupikia, ukiwa na lengo la kuonesha uwezekano wa teknolojia hiyo kuwa miongoni mwa njia mbadala za nishati safi ya kupikia, salama na rafiki kwa mazingira.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bora Women Go Green, Dkt. Bora Haule, amesema maandalizi ya mwisho ya mradi huo yanaendelea na kwamba uzalishaji rasmi unatarajiwa kuanza mwishoni mwa Oktoba 2026.
Amesema mradi huo utakapokamilika utawezesha jamii kuona kwa vitendo matumizi ya Haidrojeni ya Kijani katika kupikia, huku ukitoa fursa ya kujifunza kuhusu teknolojia hiyo pamoja na fursa za kiuchumi zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi yake.
Mradi huo wa Haidrojeni ya Kijani Kilwa unaongeza wigo wa teknolojia zinazoweza kuchangia juhudi za Serikali za kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, hususan kupitia Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia 2024–2034.
Mkakati huo umeweka lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034. Hivyo, teknolojia bunifu kama Haidrojeni ya Kijani zinaweza kuwa sehemu ya wigo mpana wa suluhisho zinazolenga kufikia lengo hilo.
Kwa ujumla, mradi huo unaonesha nafasi ya teknolojia na ubunifu katika kuongeza chaguo la nishati safi ya kupikia, sambamba na kuchangia juhudi za kupunguza matumizi ya nishati zinazochafua mazingira na kuboresha afya na ustawi wa wananchi.







No comments:
Post a Comment