WAZIRI KAPINGA AKAZIA UMUHIMU WA BRELA KATIKA UBORESHAJI WA BIDHAA NA UKUAJI WA BIASHARA NCHINI - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Monday, October 26, 2026

WAZIRI KAPINGA AKAZIA UMUHIMU WA BRELA KATIKA UBORESHAJI WA BIDHAA NA UKUAJI WA BIASHARA NCHINI


NA MWANDISHI WETU


Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameitaja Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kuwa mdau muhimu katika juhudi za Serikali za kuongeza thamani ya mazao, kuboresha bidhaa za wajasiriamali na kukuza biashara nchini, akisisitiza umuhimu wa kuwafikishia wafanyabiashara huduma za usajili na ulinzi wa miliki bunifu.


Amesema hayo Oktoba 24, 2026, wakati akifungua Maonesho ya Kitaifa ya Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) yanayofanyika Kahama, mkoani Shinyanga, ambapo alitembelea mabanda ya washiriki na kukagua bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na wajasiriamali.


Amesema wakati wa ziara hiyo alibaini kuwa baadhi ya wafanyabiashara wanashiriki maonesho hayo bila kuwa na alama za biashara zinazotambulisha bidhaa zao, hali inayodhihirisha umuhimu wa BRELA kuimarisha utoaji wa elimu na huduma za usajili wa alama za biashara na huduma ili kuwawezesha wajasiriamali kulinda na kukuza bidhaa zao.


“Lengo la kushiriki maonesho haya ni kutoa huduma kwa washiriki pamoja na wananchi wanaotembelea maonesho. Ni muhimu kuhakikisha kuwa ifikapo mwisho wa maonesho haya, wajasiriamali wamepata huduma zinazowawezesha kutambulisha na kulinda bidhaa zao, na hivyo kuimarisha utambulisho wa bidhaa za Tanzania,” alisema Kapinga.


Aidha, Waziri Kapinga amesisitiza kuwa BRELA inapaswa kuendelea kubuni njia bora za kuwafikishia wajasiriamali huduma zake, ikiwemo kuwahudumia katika maeneo wanayofanyia biashara, badala ya kutegemea wafanyabiashara kuacha shughuli zao na kufika ofisini kupata huduma.


“Ni vigumu kwa wajasiriamali kuacha shughuli zao za kila siku na kwenda ofisini kutafuta huduma. Hivyo, BRELA inapaswa kutafuta namna bora ya kuwafikia na kuwahudumia wajasiriamali ili kuwawezesha kuboresha bidhaa zao na kukuza biashara zao,” alisisitiza Waziri Kapinga.


Ameeleza kuwa Tanzania ina utajiri wa rasilimali mbalimbali, zikiwemo mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini, ambazo zinaweza kutumika kama malighafi katika uzalishaji wa bidhaa zenye thamani kubwa. Hivyo, amehimiza rasilimali hizo kuchakatwa ndani ya nchi ili kuongeza thamani yake, kukuza viwanda na kutengeneza fursa zaidi za ajira na biashara.


Alibainisha kuwa kuongeza thamani ya rasilimali za ndani kutaiwezesha nchi kunufaika zaidi na uzalishaji wake, kupanua wigo wa masoko na kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kitaifa, kikanda na kimataifa.


Katika kutekeleza agizo la Waziri Kapinga la kuwahudumia washiriki, BRELA inatumia maonesho hayo kuwafikia wajasiriamali na kutoa elimu pamoja na huduma za papo kwa papo zinazohusu usajili wa majina ya biashara, kampuni, alama za biashara na huduma, pamoja na utoaji wa leseni za viwanda na leseni za biashara zilizo chini ya mamlaka yake.


Usajili wa majina ya biashara na kampuni ni hatua muhimu katika kuwawezesha wajasiriamali kuendesha shughuli zao katika mfumo rasmi, kujenga utambulisho wa kisheria wa biashara zao na kuweka msingi wa kupanua shughuli zao. Hatua hiyo pia hufungua fursa za kuimarisha ushirikiano wa kibiashara, kuvutia uwekezaji na kuongeza uwezo wa biashara kukua.


Vilevile, usajili na ulinzi wa alama za biashara na huduma huwasaidia wajasiriamali kutofautisha bidhaa zao na za washindani, kujenga utambulisho unaotambulika sokoni na kuimarisha imani ya wateja. Hili ni muhimu hasa kwa wajasiriamali wanaoongeza thamani ya mazao ya ndani na wanaolenga kuingia katika masoko mapya.


Naye Afisa Usajili kutoka taasisi hiyo Bw. Selemani Selemani amesema msisitizo wa Serikali katika kuongeza thamani ya rasilimali za ndani unaweka umuhimu wa kuunganisha uzalishaji wa malighafi, uchakataji, urasimishaji wa biashara, ulinzi wa miliki bunifu na upatikanaji wa masoko. Ushirikiano huo unaweza kusaidia biashara ndogo kukua na kuwa biashara imara zenye uwezo wa kushindana katika soko.


“BRELA inaendelea kuchangia uboreshaji wa mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, sambamba na juhudi za Serikali za kuimarisha sekta binafsi, kukuza viwanda na kuongeza matumizi yenye tija ya rasilimali zinazopatikana nchini.


Kwa ujumla, kuongeza thamani ya malighafi zinazozalishwa nchini kunatarajiwa kuchochea ukuaji wa viwanda, kuongeza fursa za ajira, kukuza biashara za ndani na kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko mbalimbali. Urasimishaji wa biashara ni miongoni mwa hatua zinazoweza kuwawezesha wajasiriamali kunufaika zaidi na fursa hizo” amesema Bw. Selemani.


Maonesho ya SIDO Kitaifa yanafanyika kuanzia tarehe 21 hadi 30 Oktoba 2026 yakiwa na kaulimbiu ya Teknolojia na Soko Chachu ya Viwanda Vidogo Nchini”.



No comments:

Post a Comment