NA MWANDISHI WETU, KILIMANJARO
MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu, ameendesha harambee na kufanikisha kuchangisha Shilingi milioni 117.8 kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ushirika wa Naibili, Siha Kilimanjaro.
Pia imeleezwa kwamba fedha hizo ambazo zimechangishwa zitaenda kwenye ujenzi wa jengo jipya la ibada ambalo ujenzi wake ulianza miaka sita iliyopita, katika harambee hiyo Sh 50.2 milioni ni taslimu, Sh 66.5 ni ahadi na Sh 1.1 zilipatikana kwa njia ya mnada na mifuko 118 ya saruji ilipatikana.
Baada ya harambee hiyo ambayo umefanyika leo Oktoba 20, 2024 katika ushirika huo, kwa mujibu wa Mkuu wa Dayosisi Kaskazini ya KKKT, Dkt Fredrick Shoo, fedha ambazo zimepatikana pamoja na mifuko ya Saruji zitatumika kwenye upanuzi wa lengo la ibada na kazi ya plasta
"Kazi hizo mbili za upauzi na plasta, zinatarajiwa kugharimu kiasi cha Sh150 milioni," amesema.
Dkt. Shoo, amwongeza kuwa matamanio yao ni kuona wanakamilisha plasta, kuweka madirisha, milango na madhabahu, kupaka rangi na kuanza maandalizi ya kutengeneza samani, ifikapo mwaka 2026.
"Hadi kufikia hatua ya kabla ya upauzi, jumla ya kiasi cha Sh229.8 milioni kimetumika, shukrani kwa watu wenye mapenzi mema na Mungu kwa michango yao," amesema.
Askofu Shoo amefafanua kwamba baada ya upauzi na plasta, awamu ya pili ni kujenga madhabahu na madirisha na milango ya mbao.
Ameongeza kuwa baada ya hapo awamu inayofuata itakuwa kuweka tarazo, bodi ya dari, kusuka umeme na rangi, huku awamu ya nne ikiwa ni kuweka viti na kumalizia madhabahu kwa kutumia mbao.
Awamu ya mwisho itakuwa ni kufunga vifaa vya muziki, mifumo ya CCTV Kamera, kiyoyozi na mfumo wa TEHAMA.
“Ni wakati mwafaka wa kushirikiana kufanya kazi hii ya baraka iliyopo mbele yetu. Mungu atutie nguvu” alihitimisha Askofu Shoo.
Naye, Mchechu akizungumza na viongozi wa kidini, Serikali na kijamii, pamoja na waumini wa Naibili, amesema, ataendelea kuwa na moyo wa kutoa na kushirikiana hadi ujenzi wa nyumba hiyo ya ibada utakapokamilika.
Aidha ametoa wito kwa waumini wa kanisa hilo na wadau wengine kutoishia hatua ya kuwekwa kwa Jiwe la Pembe tu, jambo ambalo tayari imefanyika, kinachotakiwa ni kuendelea kufanya kazi kwa pamoja hadi ujenzi huo ukamilike.
“Tunapoendelea na ujenzi huu, nataka niwaombe ninyi wapendwa msiishie hapa. Tuendelee kufanya kazi kwa pamoja mpaka ujenzi utakapokamilika,” alisema.
Aliongeza: “Kanisa bado linahitaji michango yenu, maombi yenu, na utayari wenu wa kujitoa. Kila mmoja wetu anaweza kutoa kitu, iwe ni fedha, muda, au huduma kwa namna yoyote ile.”
Alisema ikiwa watatoa kwa moyo wa upendo, Mungu atarudisha zaidi na zaidi na vikombe vyao vitafurika.
Mchechu alisisitiza kwa kunukuu Biblia katika Luka 6:38: "Wapeni watu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa, cha kusukwasukwa, na kushindiliwa, na kufurika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu."
Aliongeza: “Kama vile Nehemia alivyowaongoza watu wa Yerusalemu kujenga tena ukuta wa mji baada ya kuharibiwa, ninyi pia muendelee kujitoa kwa uaminifu na bidii katika ujenzi wa nyumba ya Mungu.”
.jpg)




No comments:
Post a Comment