KITAMBULISHO KUTUMIKA UNUNUZI TIKETI TRENI YA SGR - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Friday, August 16, 2024

KITAMBULISHO KUTUMIKA UNUNUZI TIKETI TRENI YA SGR


NA HALIMA MAKANGILA

SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC),limesema abiria anayetumia usafiri wa treni ya umeme (SGR,) anapaswa kuwa na kitambulisho chenye sura ya muhusika na majina matatu yatakayoonekana kwenye tiketi.

Hayo yamebainishwa leo Agosti 16,2024, jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo Cha Habari na Mawasiliano TRC, Jamila Mbarouk na kufafanua kuwa  lengo la kufanya hivyo ni kudhibiti uhalifu wa baadhi ya abiria wanaotumia usafiri huo.

"Abiria yoyote hataweza kukata tiketi kama hatokuwa na kitambulisho chochote kinachoonesha sura yake na majina matatu yatakayoonekana kwenye tiketi, pia atakaguliwa kabla ya kuingia kwenye treni kwa kupitisha tiketi kwenye mashine na atakaguliwa tena akiwa ndani na atakaposhuka," amesema.

Amesema ukaguzi huo utasaidia kubaini abiria wanaopitiliza vituo na atakayebainika atahojiwa ikiwa atapatikana na hatia hatua kali itachukuliwa dhidi yake ikiwemo kulipa faini au kufikishwa mahakamani na tayari hatua hizo zimechukiwa kwa waliokamatwa kwa kosa hilo hilo.

Jamila ameongeza kuwa, ikiwa abiria atakuwa na abiria wengine ambao anataka kuwatia tiketi,atapaswa kwenda katika dirisha la kukata tiketi akiwa na vitambulisho vya wahusika ambao watakaguliwa kabla kuingia kwenye treni.

Amefafanua kuwa ukaguzi huyo unafanywa na Vyombo vya Ulinzi na Usalama  vya shirika hilo na kuweka wazi kuwa wamegundua kuwa vitendo visivyo vya uaminifu vimekuwa vikifanywa na baadhi ya abiria wanaopanda katika vituo vya Ruvu na Ngerengere na kuwataka kuacha vitendo hivyo kwani sheria kali zitachuliwa dhidi yao.

Ameongeza kuwa TRC katika kujiimarisha inaendelea kufanya ukaguzi wa tiketi mara kwa mara ili kuhakikisha changamoto ambazo zimetolewa na moja ya taasisi ya uchunguzi zinafanyiwa kazi vya kutosha ili kudhibiti mapato yanaweza kupotea kutokana na kuwepo kwa baadhi ya abiria wasiokuwa waadilifu.

Pia amesema TRC inaendelea kutoa elimu kwa abiria kwa kuwaelimisha kwamba treni hiyo na miundombinu yake ni mali ya watanzania hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuilinda na kuithamini kutokana na kutumia gharama kubwa katika ujenzi wake na atakayefanya kinyume hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.


No comments:

Post a Comment