WANANCHI wa Kata ya Buyuni, jijini Dar es Salaam, wameipongeza Serikali kwa kuwasogezea karibu zoezi la uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa (NIDA), huku wakiomba liwe endelevu ili kuwafikia wananchi wengi zaidi wanaohitaji huduma hiyo muhimu.
Wakizungumza mapema leo Januari 30, 2026 jijini Dar es Salaam, katika kilele cha zoezi hilo lililozinduliwa rasmi Januari 19, 2026, wananchi hao wamesema zoezi hilo limewasaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha usajili wa kupata vitambulisho vya Taifa ambavyo ni muhimu kwa huduma mbalimbali.
Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa Buyuni, Jamalidin Amri amesema zoezi la uandikishaji limekwenda vizuri na kufanikiwa kutokana na usimamizi mzuri wa viongozi wa kata pamoja na ushirikiano kutoka Serikalini.
“Tunaishukuru Serikali kwa kutuletea zoezi hili katika kata yetu. Uandikishaji umeenda vizuri na tunawashukuru viongozi wetu kwa kutusimamia ipasavyo. Hata hivyo, bado kuna wananchi wengi wanaohitaji huduma hii, hivyo tunaomba zoezi liwe endelevu,” amesema Jamalidin.
Ameongeza kuwa mahitaji ya vitambulisho vya Taifa ni makubwa kwa wananchi, hivyo kuendelea kwa zoezi hilo kutasaidia kupunguza changamoto kwa wananchi wanaokosa huduma mbalimbali zinazohitaji kitambulisho cha NIDA.
Kwa upande wake, Salama Kumbi, mkazi wa Chanika katika Kata ya Buyuni, amesema zoezi hilo limefanikiwa na kuwasaidia wananchi waliokuwa na changamoto kwa muda mrefu kupata huduma hiyo.
“Zoezi la uandikishaji wa vitambulisho vya NIDA limeenda vizuri. Nilikuwa na changamoto hapo awali, lakini leo hii nimemaliza zoezi langu. Tunawashukuru viongozi wetu kwa jitihada zao,” amesema Salama.
Naye Rehema Jabir Kibiri amesema changamoto kubwa katika utekelezaji wa zoezi hilo ilikuwa ni wingi wa wananchi na foleni ndefu, hata hivyo wananchi wengi wamefanikiwa kupata huduma hiyo.
“Tunakishukuru kiongozi wetu wa kata, Diwani Jesca Msolla, ambaye ametupambania wananchi wake kwa kuondoa usumbufu wa kufuata huduma za NIDA mbali,” amesema Rehema.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Buyuni, Jesca Msolla, amesema zoezi hilo limehitimishwa kwa mafanikio, ambapo zaidi ya wananchi 2,000 wamejitokeza kujisajili kupata huduma ya kitambulisho cha Taifa.
Amesema zoezi hilo limeweza kufikia kata nane na utekelezaji wake umeenda vizuri huku wananchi wakihudumiwa kwa ufanisi.
“Tumeweza kuwafikia wananchi wengi, lakini bado kuna uhitaji mkubwa wa huduma hii. Hivyo tumeomba mamlaka husika kuhakikisha zoezi hili linaendelea,” amesema Msolla.
Aidha, amewahasa wananchi wa Kata ya Buyuni kufuata maelekezo yote yanayotolewa na Serikali ya kata hiyo na kuepuka madalali vishoka wanaowadanganya wananchi kwa madai ya kuwawezesha kupata huduma mbalimbali zinazoletwa katika kata hiyo.








No comments:
Post a Comment