NA MWANDISHI WETU
MAHAKAMA Kuu ya Zanzibar imemhukumu Khadija Shabani Ali (35), mkazi wa Chukwani, kifungo cha miaka 20 " Chuo cha Mafunzo" kutokana na kupatikana na hatia ya kumchoma kwa kisu mke mwenza wake, Maymuna Said Suleiman.
Kwa mujibu wa hati ya mahakama, tukio hilo lilitokea Februari 9, 2025 saa saba mchana katika eneo la Chukwani, kwa mshtakiwa kumshambulia mke mwenzake kwa kisu na kumjeruhi katika maeneo kadhaa ya mwili ikiwemo paji la uso.
Awali, Khadija Shabani Ali alifikishwa mahakamani akikabiliwa na shtaka la kujaribu kuua, kinyume na kifungu cha 193(b) cha Sheria ya Adhabu namba 6 ya mwaka 2018.
Mahakama ilielezwa kuwa upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi 10, akiwemo mlalamikaji mwenyewe, ambao ushahidi wao uliisaidia mahakama kufikia uamuzi wa kumpata mshtakiwa na hatia bila shaka.
Baada ya kusikiliza hoja zote, mahakama ilitoa adhabu ya kifungo cha miaka 20, ikisisitiza kuwa adhabu hiyo inalenga kutoa funzo kwa jamii na kudhibiti vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyoendelea kujitokeza.
Hukumu hiyo imetolewa leo 30 Januari 2026 na Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Mheshimiwa Aziza Iddi Suwedi, baada ya mahakama kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.
%20(1).jpeg)




No comments:
Post a Comment