MFUMO WA PAIS KUDHIBITI MIGOGORO BAINA YA WANYAMAPORI NA BINADAMU BABATI - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Tuesday, October 22, 2024

MFUMO WA PAIS KUDHIBITI MIGOGORO BAINA YA WANYAMAPORI NA BINADAMU BABATI


Mkuu wa wilaya ya Babati,Emmanuela Kaganda akifungua   mafunzo ya mfumo wa PAIS wa kudhitibi migogoro ya  binaadamu na wanyamapori

NA MWANDISHI WETU, BABATI

ADHA  ya wananchi wa wilaya ya Babati,Mkoa Manyara kuwa na migogoro baina ya wanyamapori na binaadamu imepata tiba baada ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuja na mfumo wa usimamizi wanyama wakali na waharibifu(PAIS).


Katika mfumo huo, unawezesha wananchi kutoa taarifa haraka za uwepo wa wanyama wakali na waharibifu katika maeneo yao na zitawafikia maafisa wa Wanyamapori na kuchukuliwa hatua za haraka.


Mfumo huo pia unarahisisha kuandika madai ya uharibifu wa wanyamapori,Uhakiki na malipo ndani ya muda mfupi tofauti na miaka ya nyuma.


Akifungua mafunzo ya viongozi wa Serikali katika eneo la Ikolojia ya Manyara-Tarangire,Mkuu wa wilaya ya Babati Emanuela Kaganda alisema mfumo huo ukitumika vizuri utapunguza sana migogoro baina ya wanyamapori na Binaadamu wilayani Babati.


"Nawapongeza  sana Wizara ya Maliasili na Utalii  kwa kuja na mfumo huu  ambao unawezesha kudhibitiwa uharibifu wa mazao ama madhara ya wanyamapori kabla haujatokea na nawapongeza chemchem kwa kuwezesha kufanyika mafunzo haya "alisema


 Kaganda ameaema mfumo huo ,unarahisisha pia  mchakato wa kutoa mkono wa pole kwa wananchi watakao pata athari za wanyama .

 

Ameongeza kuwa mfumo huo utakuwa na faida kubwa kama viongozi wakiujua na hivyo kuwaelimisha wananchi vijijini.


"Serikali inataka migogoro baina ya wanyamapori na binaadamu imalizwe na tunaimani mfumo huu itasaidia sana kupunguza migogoro hii"alisema


Akitoa mafunzo ya mfumo huo, Ofisa TEHAMA  mwandamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Kelvin Mtei  alisema mfumo huo ni rahisi sana na utakuwa na manufaa makubwa.


Mtei amesema mfumo huo umeunganishwa na   Mkurugenzi wa Wanyamapori, Mamlaka ya usimamizi wanyamapori(TAWA) ,Shirika la hifadhi za Taifa(TANAPA) Wakala wa misitu (TFS) na Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro(NCAA).


"Mfumo huu unawezesha mwananchi kutuma taarifa kupitia simu ya mkono kwa haraka na hivyo kudhibitiwa wanyamapori"alisema


Ofisa Wanyamapori kutoka wizara ya Maliasili na Utalii, Hamisi Ashery amesema mfumo huo ni rafiki na utawezesha sasa malipo ya vifuta machozi kutolewa kwa wakati.


"Mfumo huu ukiingia unaonesha kila jambo ambalo unahitaji na unapunguza  sana kazi za maafisa wanyamapori,maafisa kilimo ma wengine kufanya tathmini za uharibifu na kuandika madai"alisema



Naye Ofisa Ujirani mwema katika hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara,Maingo ole Kili amesema mfumo huo ni suluhu ya migogoro baina ya wanyamapori na binaadamu


Mafunzo ya mfumo huo yamedhaminiwa na taasisi ya Chemchem association ambayo imewekeza  shughuli za uhifadhi na Utalii katika eneo la hifadhi ya jamii ya wanyamapori ya Burunge wilayani Babati, mkoani Manyara.





No comments:

Post a Comment