NA MWANDISHI WETU
ZAIDI ya shilingi trilioni 2.7 zinatarajiwa kutumika kujenga barabara za 10 mzunguko kwa njia ya ubia katika Mkoa wa Dar es Salaam hali ambayo itapunguza foleni na kuokoa asilimia 20 fedha zinapotea.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia wa Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila katika taarifa yake aliyotoa kwa vyombo vya habari mwishoni mwa wiki.
Kafulila alisema Serikali inafanya mazungumzo na kampuni ya China Overseas Engineering Group Co. Ltd. (COVEC) ambayo imeonesha nia kuwekeza Dola za Marekani bilioni 1 (zaidi ya Shilingi trilioni 2.7) kujenga barabara zenye lengo la kupunguza kero ya foleni jijini Dar es Salaam.
Alisema Kampuni ya COVEC inataka kutekeleza mradi huo wa kimkakati kwa njia ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), hivyo serikali ipo katika hatua mbalimbali za mazungumzo.
Kafulila, amesema kuwa mwekezaji huyo tayari amefanya kazi za awali, kama vile upembuzi yakinifu na uchambuzi wa kiuchumi.
Alisema Kampuni ya COVEC inataka kuingia katika Hati ya Makubaliano (MOU) na Serikali ili iweze kufanya upembuzi yakinifu wa mradi huo.
"Kampuni ya COVEC inataka kujenga barabara 10 za mazunguko kupunguza foleni jijini Dar es Salaam.Barabara hizo za mazunguko ni pamoja na sita za ndani na nne za nje,".
Kafulila alisema utafiti uliofanywa na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) mwaka 2020 umebaini kuwa foleni inasababisha biashara kupoteza asilimia 20 za faida zao kutokana na foleni za magari kwenye barabara jijini Dar es Salaam.
Alisema Dar es Salaam ni moja ya miji inayokuwa kwa kasi zaidi barani Afrika na hivyo kukumbwa na kero kubwa ya foleni, hususan nyakati za asubuhi na jioni.
"Kukamilika kwa ujenzi wa barabara hizo kunatarajiwa kupunguza foleni kwenye barabara kuu za Dar es Salaam, kwani magari yataweza kutumia barabara za kuzunguka zenye malipo," alisema.
Mkurugenzi huyo alisema kampuni ya COVEC ya China ina uzoefu wa kujenga miradi ya miundombinu mikubwa na ya saizi ya kati kwenye takribani nchi 100 duniani, yenye jumla ya thamani ya Dola za Marekani bilioni 12.22.
Miradi iliyotelekezwa na kampuni hiyo inayokamilikiwa na Serikali ya China ni pamoja na ujenzi wa barabara, nyumba, madaraja, miradi ya maji, umeme na sekta nyingine.






No comments:
Post a Comment