SERUKAMBA AKOSHWA NA WCF KULINDA NGUVU KAZI - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Thursday, October 31, 2024

SERUKAMBA AKOSHWA NA WCF KULINDA NGUVU KAZI


NA MWANDISHI WETU, IRINGA

MKUU wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba, ameupongeza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa juhudi zake za kulinda nguvu kazi ya taifa kupitia ulipaji wa mafao kwa wafanyakazi wanaokumbana na ajali au magonjwa yanayotokana na kazi.


Akifungua mafunzo kwa madaktari kutoka mikoa ya Iringa, Njombe, Songwe, Rukwa, Mbeya, Katavi, na Ruvuma, Serukamba alisisitiza umuhimu wa mafunzo hayo katika kuwajengea madaktari uelewa wa taratibu za kuwahudumia wanufaika wa WCF.


Alisema mafunzo hayo yatasaidia kufanya tathmini sahihi ya athari za kibaolojia zinazotokana na ajali za kikazi na magonjwa, akiwataka madaktari kuhakikisha wafanyakazi wanapata huduma zinazostahili na kulipwa fidia kwa wakati.


Akizungumza kwenye mafunzo hayo Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dk John Mduma alisisitiza umuhimu wa waajiri wote kujiunga na mfuko huo kama sheria inavyotaka. 


Alieleza kuwa lengo la mfuko ni kulipa mafao kwa wafanyakazi wanaopata ajali au magonjwa kutokana na kazi, pamoja na kutoa fidia kwa wategemezi wa wafanyakazi wanaofariki.


"Ili kuhakikisha wanufaika wanapata huduma bora za afya, WCF imekuwa ikitoa mafunzo kwa madaktari nchi nzima. Hadi sasa, madaktari 1,606 wamepata mafunzo ya awali, na wengine 133 wamepata mafunzo kwa vitendo," amesema.


Dk Mektilda Emmanuel kutoka Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Songwe, ambaye ni mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo, amesema semina hiyo itamuwezesha kupata ujuzi wa kuwasaidia watu wanaokabiliwa na changamoto za kiafya wakiwa kazini.


Naye Dk Baraka Mponda kutoka Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya, amesema  mafunzo hayo yamemsaidia kuongeza uwezo wa kufanya tathmini ya wagonjwa walioathirika na magonjwa yanayotokana na kazi zao.



No comments:

Post a Comment