NA MAGENDELA HAMISI
RAIS wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, anatarajia kufungua Mkutano wa Sita
wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini utakaoanza Novemba 19 mwaka
huu jijini Dar es Salaam na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dkt Hussein Alli Mwinyi ataufunga Novemba 21, 2024.
Aidha Mkutano huo
mkubwa wa Madini unatarajiwa kuudhuriwa na washiriki zaidi ya 1,500 kutoka mataifa
mbalimbali Duniani ambapo wataalamu, Mawaziri, mabalozi watafiti watashiriki
mkutano huo na watajadili mada nane kutoka watoa mada 20 wa kimataifa na 35 wa
hapa nchini ambao wamebobea kwenye sekta ya madini.
Waziri wa Madini
Antony Mavunde, amebainisha hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na
waandishi wa habari na kufafanua kuwa kwa mdau anayetaka kushiri anaweza
kujisajili kupitia tovuti ya mkutano ambayo ni conference.madini.go.tz.
“Tunamshukuru Rais
Dk. Samia kupitia mikakati yake amefanikisha sekta ya madini kupiga hatua kibwa
kimafanikio na sasa inachangia katika pato la taifa asilimi tisa na mkakati
ambao upo kwa sasa ifikie asilimia 10 na Novemba 19 atafungua mkutano huo na
utafungwa na Rais wa Zanzibar Dkt Mwinyi,” amesema.
Ameongeza kuwa
wadau mbalimbali wataudhuria mkutano huo wakiwemo, Watendaji Wakuu wa kampuni
kubwa za madini duniani ambazo zinatarajia kuwekeza nchini, ikiwemo Kampuni ya
Barrick Gold, AngloGold Ashanti, Life Zone Metals, ShantaGold, Eco Graph, Faru
Graphite, HeliumOne, Lindi Jumbo, Sotta Mining.
Pia amesema wengine
watakaokuwemo ni watafiti, mabalozi 31 wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini na
wanaoiwakilisha nchi yetu nje ya nchi akiwemo Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Umoja wa Mataifa, Balozi Hussein Kattanga,
Mashirika ya Kimataifa, waongezaji thamani madini, wafanyabiashara, taasisi za
fedha, Vyuo Vikuu na Vya kati, Taasisi za umma na binafsi zinazojihusisha na
shughuli za madini, viongozi mbalimbali wa kitaifa kutoka wizara, Taasisi,
Mikoa, Halmashauri na Idara za Serikali.
Waziri Mavunde amesema mkutano huo amewahamasisha wadau na watanzania kutumia
fursa ya uwepo wa mkutano huo kujifunza, kufuatilia na kushiriki ili kuijenga
uchumi wa nchi kupitia shughuli mbalimbali katika mnyororo wa thamani kwenye
sekta ya madini.
Ameweka wazi kwamba
mkutano huo unalenga si tu kuvutia uwekezaji, bali pia kuweka msingi thabiti wa
ushirikiano baina ya wadau, kuimarisha uzalishaji wa madini, na kuhakikisha
kuwa rasilimali hizi zinawanufaisha watanzania kiuchumi na kijamii.
Mada
zitakazojadiliwa zitagusia maeneo mengi ikiwemo changamoto zinazokabili masuala
ya uongezaji thamani madini, fursa za uwekezaji na mitaji kwenye sekta ya
madini; mikakati ya uendelezaji madini mkakati kwa ajili ya kuongeza manufaa ya
mnyororo wa thamani, matumizi ya teknolojia katika uchimbaji mdogo wa madini;
ushiriki wa wanawake na vijana katika Sekta ya madini, kuendelea kutangaza
madini adimu ya Tanzanite, na masuala mengine yakiwemo uchimbaji bora na
uhifadhi wa mazingira.
Mkutano huo utaongozwa na kaulimbiu isemayo “Uongezaji thamani Madini kwa
maendeleo ya kiuchumi na kijamii”, ambayo inalenga kuhimiza umuhimu wa
uongezaji thamani wa madini kama njia ya kuleta faida zaidi za kiuchumi na
kijamii kwa maendeleo endelevu ya taifa letu na dunia.
Pia utakuwana
mkakati wa kupandisha thamani ya madini yanayozalishwa nchini kabla ya
kusafirishwa nje kwa lengo la kuchochea uanzishwaji viwanda vitakavyokuwa na manufaa
nchini, kwa majirani wanaotuzunguka na duniani.
Ameongeza kuwa Novemba 20, 2024 kutakuwa na hafla ya usiku wa madini
itakayofanyikakuanzia Saa 12.30 Jioni na mgeni rasmi atakuwa ni
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati wa Tanzania, Dkt. Doto Biteko.
Wazizri Mavunde ametanabaisha kuwa katika hafla hiyo kutakuwa na tukio maalum
la kutambua mchango wa wadau waliofanya vizuri katika sekta ya madini kupitia
makundi mbalimbali.
Pia hafla hiyo
inalenga kutambua mchango wa wadau hawa katika maendeleo na ukuaji wa sekta,
huku ikihamasisha wadau wengine kuongeza juhudi, kuziona fursa zilizopo na
kuchangia katika mafanikio ya sekta ya madini nchini. Pia, usiku wa madini
huambatana na onesho la bidhaa za madini ya vito.
Amesema mkutano huo
ni mwendelezo wa mikutano mingine iliyotangulia tangu kuanza kwake mwaka 2019
ambapo Serikali ilitenga zaidi ya saa sita kusikiliza kero, changamoto na maoni
kutoka kwa wadau wa madini.
"Kutokana na
matokeo ya mkutano ule wa Mwaka 2019, Serikali iliona umuhimu wa kuwa na
mikutano huu yenye sura ya Kimataifa na hivi sasa, imevuka mipaka ya nchi yetu
ikihusisha wadau kutoka ndani na nje ya Tanzania wanaohusika katika mnyororo
mzima wa shughuli za madini.
"Kama
mnavyofahamu kwamba, nchi yetu ya Tanzania imejaliwa utajiri wa aina mbalimbali
za madini kutoka makundi karibu yote ya madini yakihusisha madini ya metali,
madini mkakati, madini ya viwandani, vito vya thamani kubwa, madini
yanayopatikana chini ya sakafu ya bahari kuu, ambayo yote yanaifanya Tanzania kuwa
miongoni mwa nchi wazalishaji wakubwa wa madini yanayohitajika duniani kote.
Kwa muktadha huo,
Serikali kupitia Wizara ya Madini iliona upo umuhimu wa kuwa na jukwaa
moja linalowaleta pamoja wadau kutoka pande mbalimbali za nchi
kusikia kutoka kwetu moja kwa moja kuhusu uwepo wa rasilimali hizi ambapo
ikiwa zitatumika vizuri zinaweza kuibadili kiuchumi na kijamii Nchi yetu ya
Tanzania na kuifanya moja ya Nchi zinazozalisha kwa wingi madini
duniani." Ameeeleza
Amesema mkutano huo
unafanyika kila mwaka ili kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kuendelea
kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.
Pia ni jukwaa la
kujadili kwa pamoja mustakabali wa sekta ya madini, kushirikishana maarifa,
ujuzi na kuangazia fursa mpya zinazojitokeza katika sekta hii inayokua kwa
kasi.
Aidha mkutanmo huo unatoa
nafasi kwa washiriki kujifunza kuhusu Sera na mikakati mipya ya serikali,
kujadili masuala ya kisheria na kiuchumi yanayohusiana na madini, na kushuhudia
teknolojia mpya na ubunifu unaoweza kuleta thamani zaidi katika utafiti,
uchimbaji na uongezaji thamani wa madini kupitia mawasilisho na maonesho
kwenye mabanda yanayoenda sambamba na mkutano.










No comments:
Post a Comment