NA JOHN MAPEPELE
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imesema imeona thamani ya fedha ambayo Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imewekeza kwenye sekta ya misitu na nyuki.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Timotheo Mnzava (Mb) amesema haya leo Novemba 13, 2024 wakati anahitimisha ziara ya kikazi mkoani Tabora kwenye kiwanda cha kuchakata mazao ya nyuki cha Nkiniziwa wilayani Nzega baada ya kukagua miradi mbalimbali ya sekta ya misitu na nyuki huku akitaka juhudi zaidi za kutangaza ziongezwe.
Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Prof Dosantos Silayo amesema mradi wa kiwanda hicho umefadhiliwa na Mfuko wa Misitu Tanzania na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ambapo hadi kukamilika umegharimu takribani shilingi milioni 295
Kamati imeielekeza Wizara kwa kushirikiana na wadau kuendelea kuanzisha vikundi vya wajasiliamali na viwanda vya mazao ya misitu na nyuki ili uzalishaji uongezeke na kupanua ajira kwa wananchi.
Katika ziara hiyo Kamati iliambatana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula (Mb), Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi na baadhi ya Watendaji wa Wizara na taasisi zilizo chini ya Wizara.
Aidha, Mhe. Mnzava amesema sekta za misitu na nyuki zina mchango mkubwa kwa jamii hivyo ni muhimu kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi hiyo.
Amefafanua kuwa endapo sekta ya misitu na nyuki itasimamiwa kikamilifu ina mchango kwenye uhifadhi wa Maliasili kwa kuwa watu wataacha tabia za kuharibu misitu na mazingira kwa ujumla.
Ameitaka Wizara kuendelea kuwekeza kwenye elimu ya namna bora ya kufuga nyuki na kuvuna asali kwa njia bora ili kupata bidhaa zenye ubora zitakazopenya kwenye masoko ya kimataifa.
Miradi hiyo inatekelezwa katika Wilaya zote 7 za Mkoa wa Tabora ambazo ni Tabora, Uyui, Nzega, Igunga, Sikonge, Urambo na Kaliua.
Naye Mhe. Kitandula kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi. Dkt. Pindi Chana ameishukuru kamati kwa ushauri na maelekezo iliyoyatoa na kuahidi kuyatekeleza kikamilifu.
Mara baada ya kuhitimisha ziara hiyo, Mhe. Mnzava amepanda mti katika eneo la kiwanda ikiwa ni ishara ya kuendeleza uhifadhi.










No comments:
Post a Comment