WAZIRI ULEGA KUWAPIMA MAMENEJA KWA UWEZO WA KUTATUA CHANGAMOTO WAKATI WA DHARURA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Friday, January 3, 2025

WAZIRI ULEGA KUWAPIMA MAMENEJA KWA UWEZO WA KUTATUA CHANGAMOTO WAKATI WA DHARURA


NA MWANDISHI WETU

WAZIRI  wa Ujenzi Abdallah Ulega amesema atawapima mameneja wa Wakala wa barabara nchini (TANROADS ), kwa uwezo wa kutatua changamoto  wakati wa dharura ili kuhakikisha barabara zote nchini zinapitika wakati wote. 

Ameyasema hayo leo wakati akizungumza  na wananchi wa wilaya za Handeni na Kilindi alipokagua ujenzi wa barabara ya Handeni-Mafuleta KM 20 mkoani Tanga.

Amesema Meneja anayehakikisha barabara za mkoa wake zinapitika vizuri bila msongamano na kutatua kero za watumiaji wa barabara ndiye atahesabika kuwa meneja mzuri. 

"Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amenituma  nipite kukagua miradi inayoendelea  na iliyokwama ili niikwamue ", amesema  Waziri Ulega.

Amemtaka  Mkandarasi Henan Highway Engineering Group (HEGO), anayejenga  sehemu ya Handeni -Mafuleta kuendelea kufanyakazi kwa bidii kwani ameshaanza kulipwa na ataendelea kulipwa ili aendelee kuijenga barabara hiyo usiku na mchana kwa ubora uliokusudiwa. 

"Kila mahala kwenye nchi hii kuna ujenzi unaendelea , Rais amedhamiria kuifungua nchi hii katika sekta zote ili kukuza uchumi wa watu", amesisitiza  Ulega.

Katika hatua nyingine Waziri Ulega amehimiza uharaka katika zoezi la kubaini maeneo yenye milima na kona kali katika barabara ya Segera-Chalinze ili zijengwe barabara wezeshi ili kupunguza msongamano na ajali.

" Vifo na ulemavu vimeendelea kupoteza watu kutokana na ajali za barabarani hivyo kamilisheni upembuzi yakinifu ili ujenzi katika maèneo korofi uanze mara moja", amesema  Waziri Ulega.

Naye Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Mohamed Besta amemhakikishia Waziri Ulega kufanyiakazi maelekezo yake na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi  kulinda alama za barabarani.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Handeni Albert Msando amesema  barabara ya Handeni-Singida  ni moyo wa uchumi wa  wananchi wa Handeni na Kilindi kwani ni muhimu katika shughuli za usafiri na usafirishaji  hivyo kukamilika kwake kutachochea uchumi wa wilaya za Handeni na kilindi na kuunganisha mkoa wa tanga na mikoa ya kati, kanda ya ziwa. 

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilindi Mohamed Kumbi amemhakikishia Waziri Ulega kuwa maendeleo yaliofanywa na Serikali katika Wilaya hiyo ni mengi na wataendelea kuiunga mkono Serikali ili kufikia  lengo.

Barabara ya Handeni-Mafuleta ni sehemu ya barabara kuu ya Handeni -Kiberashi -Singida yenye urefu wa KM 434.33 inayounganisha mkoa wa Tanga na mikoa ya Kati na kanda ya ziwa kukamilika kwake kutaleta tija kwa bandari ya Tanga.





No comments:

Post a Comment