NA MWANDISHI WETU
MSAJILI amefuta kampuni 11 kutokana na kukiuka masharti ya kifungu cha 400A(1) (e) Cha sheria sura 212 kuanzia Feb 27, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam leo Machi 5 2025, Msajili wa Biashara Godfrey Nyaisa, amesema kwamba kampuni hizo zimekiuka masharti kwa kufanya shughuli za kibiashara tofauti na madhumini yaliyoainishwa katika katiba za kampuni za miongozo ya uendeshaji wake wakati wa usajili
Kifungu hiki Cha sheria kikikiukwa kinampa Msajili hatua za kuchukua ikiwemo kuijurisha kampuni husika kuhusu ukiukwaji wa sheria na hatua anazokusudia kuchukua ikiwa itashindwa kutoa maelezo au yasiyoridhisha.
Ameongeza kuwa Kwa mujibu wa kifungu hicho cha sheria, alizijulisha kampuni husika kusudio la kuzifuta kupitia notisi zilizotolewa kati ya Jan 2 na 26 mwaka huu.
Amefafanua kuwa kutokana na kampuni hizo kutowasilisha maelezo yoyote kama zilivyotakiwa chini ya kifungu cha 400A (2), Msajili amezifuta rasmi na hatua nyingine za kisheria zimeanza kuchukuliwa na vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa wahusika ikiwemo kuwatia nguvuni.
"Napenda kuwasisitiza kwamba hakuna kampuni na wahusika wake watakaokuwa salama ikiwa watakiuka sheria na taratibu wa usajili wa kampuni, kampuni yoyote ile itakayofanya shughuli zake kinyume na sheria na utaratibu itashughulikiwa ipasavyo na vyombo vya usalama.
Nyaisa amezitaja kampuni hizo kuwa ni LBL Mtwara, Media Company Ltd (Na 181289972), LBL Morogoro Media Company Ltd (Na 179770873), LBL Geita Advertising Media Ltd (Na 180439242), LBL Mbeya Ltd (Na 179978326), LBL Mbezi Advertising Media Company Ltd (Na 180582835),
Nyingine ni LBL Future Vision Advertising Agency Company Ltd (Na 181302256), LBL Ubungo Media Ltd (Na 180960333), LBL Mabibo Media Company (Na 181117346), LBL Mbagala Media Company Ltd (Na 181248874), LBL Gongolamboto Media Advertising Company Ltd (Na 181513438) na LBL Dar es Salaam Kigamboni Advertising Ltd (Na 180046992).
Pia amesisitiza kwamba hakuna sheria wala taasisi yenye mamlaka ya kutoa vibali au leseni za kufanya biashara za upatu hapa nchini na kuweka wazi kwamba kampuni nyingine zinazojihusisha na biashara nje ya katiba yao, zinaendelea kufuatliwa na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufutwa kwenye rejista ya kampuni.
Pia Msajili anawakumbusha wananchi kwamba, biashara ya upatu ni kinyume cha sheria za nchi, hivyo jamii imehimizwa kutoa taarifa kwa Mamlaka husika zikiwemo taasisi za Kiserikali na Jeshi la Polisi ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya kampuni hizo au watu wanaojishughulisha na biashara ya upatu.
No comments:
Post a Comment