NA MWANDISHI WETU
WATUMISHI wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) wamesisitizwa kuwa na nidhamu wanapotekeleza majukumu yao ya kazi ili kuleta matokeo chanya kwa ustawi taasisi.
Hayo yamesemwa Julai 4, 2025 jijini Dar es Salaam na Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo Godfrey Nyaisa kwenye hafla ya utoaji tuzo kwa watumishi wa BRELA walifanya vizuri katika utekelezaji wa majukumu yao kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Katika hafla hiyo Nyaisa amesema kila mtumishi ni muhimu kuwa mwangalizi wa mwenza na kumdhibiti pale ambapo anaona anatekeleza majukumu nje ya utaratibu.
"Watumishi muwe mnadhibitiana wenyewe kwa wenyewe kwa kuheshimu kazi, kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo bila utendaji kazi hatutaona mafanikio yake" amesisitiza Nyaisa
Pofesa Neema Mori, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa BRELA amesema kuwa Bodi anayoiongoza inatambua mchango wa kila mtumishi katika utendaji wake na wameweza kupima mafanikio kutokana na bidii kubwa inayofanywa kwa kupata matokeo ya ukuaji wa mapato kila mwaka, kujitangaza, taswira chanya ya taasisi kwa jamii na uelewa wa wafanyabishara juu ya majukumu ya msingi ya Taasisi.
Watumishi waliopewa tuzo ya ufanyakazi bora ni Valerian Kiganza kutoka Kitengo cha Uhasibu na Fedha, Charles Kisaka kutoka Kurugenzi ya Huduma na Uwezeshaji, Athuman Makuka kutoka Kurugenzi ya Miliki Ubunifu, Rosemary Mpuya kutoka Kitengo cha Ununuzi,
Ally Mjema kutoka Kitengo cha TEHAMA, Jackline Sirili kutoka Kitengo cha Masijala ya Biashara, Lucas Mafuru kutoka Kurugenzi ya Leseni, Aziza Juma kutoka Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Umma, Selemani Selemani kutoka Kurugenzi ya Kampuni na Majina ya Biashara, Brighton Mshukuru kutoka Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani. Aziza Juma amepata tuzo ya utumishi hodari
Hafla hiyo imehitimishwa kwa watumishi wa BRELA kutoa tuzo maalum kwa Godfrey Nyaisa, Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA kwa kuboresha mazingira ya utendaji kazi, kuweza kusimamia na kuongoza Taasisi kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni za Kiutumishi.
![]() |
No comments:
Post a Comment