NA MWANDISHI WETU, SWEDEN
BALOZI wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyi, amempongeza mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Dkt. Samia ya jijini Dodoma, Miriam Shangali, kwa kushinda tuzo ya kimataifa ya Young Courage Award ya mwaka 2025.
Akizungumza na mwanafunzi huyo ubalozini Stockholm, Balozi Matinyi alimpongeza kwa kuonesha ubunifu, juhudi, huruma na uongozi kwa wanafunzi wenzake nchini kiasi cha kutambuliwa kimataifa akiwa kijana pekee kutoka barani Afrika aliyepokea tuzo hiyo.
Mwanafunzi huyo ameshinda tuzo hiyo inayotolewa na asasi za Raoul Wallenberg Academy kwa kushirikiana na Swedish Institute kufuatia mchango wake katika kuboresha mazingira ya hedhi salama kwa wasichana kupitia ubunifu wa taulo za hedhi za kufua.
Miriam ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha sita wa masomo ya sayansi, alibuni taulo maalum za hedhi kwa kutumia rasilimali ya gharama nafuu na kuleta mabadiliko makubwa kwenye afya na mahudhurio shuleni ya wenzake huku akitoa elimu hiyo yeye binafsi na kuzisambaza taulo hizo rafiki kwa mazingira.
Akielezea juhudi zake, alisema alichukua hatua hiyo kutokana na usumbufu alioupata yeye mwenyewe wakati akiwa kidato cha kwanza. Miriam alitunukiwa tuzo hiyo kwenye hafla iliyofanyika tarehe 27 Agosti, 2025 jijini Stockholm.
Tuzo hizo hutolewa kwa vijana wenye umri kati ya miaka 13 – 20, walioonesha ujasiri na kufanya ubunifu kwenye sekta mbalimbali kwa lengo la kubadili maisha ya jamii zinazowazunguka. Kwa mwaka huu, tuzo hizo zimetolewa kwa vijana 12 kutoka mataifa 11 ya Australia, Canada, Greece, Hungary, Monaco, New Zealand, Norway, Poland, Serbia, Sweden (2) na Tanzania.
No comments:
Post a Comment