MGOMBEA urais kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo, ameendelea na ziara zake za kampeni zinazofanyika kwa mfumo wa kufikia na kuwafata wapiga kura popote walipo, kwa mtindo wa kampeni za kijiji kwa kijiji na kata kwa kata.
Akiwa njiani kuelekea Arusha, Doyo alipita Kata ya Makuyuni, lakini pia alizungumza na wananchi wa Kata ya Meserani, Wilaya ya Monduli. Katika hotuba yake, aliwaeleza wananchi kuwa mikataba ya madini iliyosainiwa na serikali ya Chama cha Mapinduzi imekuwa ikifanyika kwa usiri mkubwa, bila Watanzania kuonyeshwa manufaa wanayoyapata kutokana na mikataba hiyo.
Doyo aliahidi kuwa, endapo atachaguliwa kuwa Rais, hatua yake ya kwanza itakuwa ni kuhakikisha anapitia upya mikataba ya madini ili kubaini kwa uwazi kile ambacho taifa linanufaika nacho.
Alisisitiza kuwa suala hilo limekuwa siri kwa muda mrefu, jambo ambalo atalivalia njuga ili kuhakikisha rasilimali za Watanzania zinabaki salama na zenye manufaa kwa wananchi.
Aidha, aliwaambia wananchi hao kuwa wanaishi jirani na Mkoa wa Manyara, hususan Wilaya ya Simanjiro, ambako kuna biashara kubwa ya madini adimu duniani, yakiwemo madini ya Tanzanite. Hata hivyo, licha ya utajiri huo mkubwa, wananchi wa maeneo ya jirani hawajanufaika ipasavyo na rasilimali hizo.
“Nimepita Makuyuni, nikawakuta ndugu zenu wakiuza pakiti za miwa na kina mama wakiuza bagia. Nikajiuliza, inaingiaje akilini kuona Watanzania wanaoishi maeneo yenye migodi ya madini ya kipekee duniani bado wakiendelea kuuza vipande vya miwa baada ya miaka 60 ya uhuru? aingii akilini,” alisema Mhe. Doyo.
Mgombea huyo amewaahidi wananchi hao kuwa, endapo watamchagua, serikali yake itajenga viwanda vya kuongeza thamani ya madini ili wananchi wa ukanda huo wapate ajira zenye staha, badala ya kuendelea kujihusisha na biashara ndogo ndogo zisizo na tija, huku wakiishi karibu na utajiri mkubwa wa Tanzanite, madini yanaolitambulisha taifa lao duniani.
Kwa sasa, msafara wa mgombea urais huyo wa Chama cha Mhe. Doyo unaelekea Arusha, Mara Mwanza.
No comments:
Post a Comment