DKT. SAMIA ALIPOVUNJA UKIMYA KUHUSU DENI LA TAIFA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Friday, October 24, 2025

DKT. SAMIA ALIPOVUNJA UKIMYA KUHUSU DENI LA TAIFA


NA MWANDISHI WETU

BAADA ya tetesi na mijadala mikali, Rais Samia Suluhu Hassan amevunja ukimya uliodumu kwa muda mrefu kuhusu ongezeko la Deni la Serikali, akitoa maelezo ya kina yanayofafanua mizizi ya deni hilo na hatua zinazochukuliwa kuhakikisha linabaki himilivu.



Kipindi cha Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete na Awamu ya Tano iliyoongozwa na Rais John Magufuli, kulikuwa na mijadala mikali kuhusu Deni la Serikali.


Hata katika Awamu hii ya Sita chini ya Rais Samia kumekuwapo mijadala ya kina na mara nyingine yenye dhana za utata kuhusu Deni la Serikali, ikijitokeza kwenye mitandao ya kijamii, mijadala ya kiuchumi ndani ya Bunge na kwenye majukwaa ya wadau wa fedha.


Mijadala hiyo imekuwa inaungwa mkono na mitazamo ya kisiasa, hasa kupitia hoja za wanasiasa wa upinzani na wachambuzi huru, ambao mara nyingi wamependekeza serikali inapaswa kutoa maelezo ya kina na ya wazi juu ya mwelekeo wa deni, ili wananchi na wadau wa fedha waelewe vigezo vya ukuaji wa deni na uhusiano wake na miradi ya maendeleo na ustawi wa uchumi wa taifa.


Akihitimisha shughuli za Bunge la 12 jijini Dodoma, Juni 27, 2025, Rais Samia amesema hadi kufikia Mei mwaka huu, Deni la Serikali lilikuwa Sh. trilioni 107.7, likijumuisha Sh. trilioni 72.9 za deni la nje na trilioni 34.8 za deni la ndani.



Rais Samia akafafanua kwamba ongezeko hilo si matokeo ya matumizi holela, bali ni sehemu ya mikakati ya Serikali kugharamia miradi ya kimkakati, ikiwamo mikopo iliyoingiwa na awamu zilizopita.


“Ni muhimu wananchi wakaelewa kuwa mikopo mingi tunayoipokea sasa ilitiwa saini katika vipindi tofauti vya serikali zilizopita. Kwa mfano, Awamu ya Sita imepokea takribani Sh. trilioni 11.3 kutoka mikopo iliyoingiwa zamani,” amesema.


Pia alieleza kuwa mikopo hiyo inalenga kuchochea maendeleo na si kuongeza mzigo wa madeni yasiyo na tija.


“Mkopo hauwi deni hadi pale fedha, huduma au vifaa vinapopokewa. Hivyo, si kila mkataba wa mkopo unamaanisha deni jipya,” alisisitiza.


SABABU ZA ONGEZEKO


Rais Samia alitaja kuimarika kwa Dola ya Marekani dhidi ya Shilingi ya Tanzania kama sababu kuu ya kuonekana kwa ongezeko la deni.



“Machi 2021 Dola moja ilikuwa sawa na Sh. 2,298.5, lakini Machi 2025 imefikia Sh. 2,650. Mabadiliko haya pekee yameongeza deni letu kwa zaidi ya Sh. trilioni 9.3 tunapolitaja kwa shilingi,” alifafanua, akisisitiza kuwa kuporomoka kwa thamani ya shilingi si dalili ya udhaifu wa uchumi, bali hatua ya kukabiliana na mitikisiko ya kiuchumi duniani.


Vilevile, Mkuu wa Nchi aliweka wazi kuhusu mwenendo wa ulipaji deni, akisema malipo yameongezeka kutoka Sh. trilioni 8.2 mwaka 2020/21 hadi makadirio ya Sh. trilioni 14.2 mwaka 2025/26.


 Ongezeko hilo, alisema, limetokana na kuiva kwa mikopo ya muda mrefu iliyochukuliwa kwa ajili ya miradi mikubwa ya maendeleo, sambamba na mabadiliko ya riba katika masoko ya fedha ya kimataifa baada ya mlipuko wa UVIKO-19.


“Baadhi ya nchi Afrika zimeshindwa kulipa madeni kwa wakati kutokana na mabadiliko haya, lakini Tanzania tumeendelea kulipa kwa uaminifu na kwa wakati,” alisema.



UWAZI, UWAJIBIKAJI


Akijibu lawama za wakosaji wake, vikiwamo vyama vya upinzani kwamba serikali yake imekopa kupita kiasi, Rais Samia alifafanua kuwa hata ongezeko la deni la ndani limetokana na uamuzi wa kulipa madeni ya zamani, hasa yale ya mifuko ya hifadhi ya jamii.


Amesema Serikali imetambua madeni yenye thamani ya Sh. trilioni 2.67 kwa mifuko ya hifadhi ya jamii ya PSSSF, NSSF na kampuni ya ubia ya mifuko ya pensheni (PPP), likiwamo deni la ujenzi wa Ukumbi wa Bunge na Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela.


“Hatua hii inalenga kunusuru mifuko ya hifadhi ya jamii na kuhakikisha wastaafu wetu wanapata mafao yao kwa wakati,” alisema Rais Samia.


Aliongeza kuwa serikali itaendelea kutambua madeni yaliyosalia ndani ya miaka mitatu ijayo, zikiwamo Sh. bilioni 630 za deni la kabla ya mwaka 1999 na Sh. bilioni 180 za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) zilizotumika kujenga Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), jijini Dodoma.



DIRA YA BAADAYE


Rais Samia aliwahakikishia Watanzania kuwa Deni la Taifa linasimamiwa kwa umakini na bado ni himilivu. “Serikali itaendelea kuimarisha ukusanyaji mapato ya ndani, kuelekeza mikopo katika miradi inayoongeza mapato na mauzo nje ya nchi na kuhakikisha maandalizi ya miradi yanazingatia sheria na miongozo,” alisema.


Alisisitiza kuwa nidhamu ya matumizi ya fedha za umma ni nguzo kuu ya serikali yake, akitaja mikakati ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kudhibiti ununuzi na kuimarisha ukaguzi wa hesabu za serikali.


Rais Samia alisema hatua zote hizo zimejikita katika kujenga uchumi imara unaotumia mikopo kwa tija. “Watanzania wanapaswa kufahamu kuwa hatukopi kwa anasa bali kwa maendeleo. Mikopo hii inalenga kutengeneza uchumi utakaowanufaisha wote, leo na vizazi vijavyo.”


SAUTI YA UTOUH



Mwandishi wa makala hii amezungumza na Ludovick Utouh, aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa miaka minane kuanzia 2006 hadi 2014, ambaye sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya WAJIBU.


Utouh, mwanazuoni wa uhasibu, anaanza kwa kutoa dhana na chimbuko la “Deni la Taifa”, akieleza kuwa ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) na malengo mengine ya kitaifa, Tanzania inalazimika kufanya uwekezaji mkubwa katika miradi ya kimkakati kama nishati, afya, elimu, maji, kilimo na maendeleo ya rasilimali watu.


Pia anasema changamoto kubwa kwa nchi zinazoendelea, ikiwamo Tanzania, ni uwezo mdogo wa kukusanya mapato ya ndani yanayotosheleza kugharamia miradi hiyo. 


“Hali hii huifanya serikali kukopa fedha ndani na nje ya nchi ili kugharamia miradi ya maendeleo. Hapo ndipo tunaposikia kuhusu “Deni la Taifa”, linalotokana na mikopo iliyochukuliwa na serikali kutoka vyanzo mbalimbali na inayotakiwa kulipwa kwa muda maalum. 


“Kwa lugha rahisi, deni hutokea pale ambapo matumizi yanazidi mapato yaliyopangwa katika bajeti ya serikali. Kwa mujibu wa Taasisi ya Kifedha ya Kimataifa (Corporate Finance Institute), Deni la Taifa ni jumla ya madeni yote ambayo nchi inadaiwa kutokana na hati fungani, dhamana au mikopo kutoka taasisi za kifedha za kimataifa kama Benki ya Dunia (WB), Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na benki za maendeleo za kikanda,” anasema.


Utouh anaeleza kuwa serikali zote duniani hukopa ili kujazia nakisi katika bajeti zao. Mikopo hii inaweza kuwa yenye masharti nafuu (concessionary) au yenye masharti magumu ya riba na dhamana. “Kwa miradi ya kimkakati inayochukua muda mrefu kukamilika, inashauriwa serikali kuchukua mikopo ya muda mrefu yenye riba nafuu,” anasema. 


Utouh anasema mikopo ya maendeleo inachochea ukuaji wa uchumi kwa kuongeza ajira, kuimarisha miundombinu na kuboresha huduma kwa wananchi. “Mara nyingi, faida ya mikopo hiyo huanza kuonekana pale miradi inayofadhiliwa inapokamilika na kuanza kuzalisha bidhaa au huduma,” anasema.


UKUAJI WA DENI


Utouh anarejea takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Zinaonesha Deni la Taifa lilikuwa Sh. trilioni 10.93 wakati Rais Benjamin Mkapa anaondoka madarakani mwaka 2005. Kufikia mwisho wa utawala wa Rais Kikwete mwaka 2015, deni hilo liliongezeka hadi Sh. trilioni 41.82, huku Pato la Taifa likikua kutoka Sh. trilioni 21.4 hadi Sh. trilioni 84.28. 


Anaeleza kuwa mwaka 2021, wakati wa uongozi wa Rais Magufuli, deni lilifikia Sh. trilioni 72.3, sawa na asilimia 53.3 ya Pato la Taifa. Kufikia Juni 2024, Deni la Taifa limeongezeka hadi Sh. trilioni 111.3, huku uchumi wa taifa ukikua hadi Sh. trilioni 230.91. 


Utouh anarejea Ripoti ya Benki ya Dunia (2023). Inaonesha uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 5.2, kulinganishwa na asilimia 4.6 mwaka 2022. Ni ishara njema kwamba deni lipo katika kiwango kinachoweza kuhimilika.


UHIMILIVU WA DENI


Utouh anasema kabla nchi haijakopa, tathmini ya uwezo wake wa kulipa hufanywa na wakopeshaji kama Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). Kwa upande wa Tanzania, tathmini ya Desemba 2023 ilionesha Deni la Taifa bado ni himilivu kwa muda mfupi, wa kati na mrefu. 


Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, uwiano wa Deni la Serikali kwa Pato la Taifa ni asilimia 35.6, chini ya ukomo wa asilimia 55 unaowekwa kimataifa.


“Hivyo, serikali ipo katika nafasi nzuri ya kuendelea kukopa kwa ajili ya maendeleo bila kuhatarisha ustawi wa uchumi,” Utouh anasema.


Anafafanua kuwa kwa viwango hivyo, Tanzania bado ina nafasi ya kukopa kwa uangalifu ili kuimarisha huduma za jamii na kuchochea ukuaji wa uchumi.


“Hatua ya serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuonesha uwazi katika matumizi ya mkopo wa Sh. trilioni 1.3 wa UVIKO-19, ni mfano bora wa uwajibikaji unaopaswa kuendelezwa na kupongezwa,” Utouh anasema.


Utouh anasema hatua hii inaweza kufanikishwa kwa kufanya marekebisho ya Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, Sura ya 134, ili kuipa sura mpya ya uwazi na ushirikishwaji wananchi


“Kwa msingi huu, Deni la Taifa si tishio, bali ni nyenzo muhimu ya maendeleo endapo litadhibitiwa kwa weledi, uwazi na uwajibikaji,” Utouh anahitimisha.

No comments:

Post a Comment