-Msanii wa muziki wa kizazi kipya anayevutiwa na Prof J
-Awataka wasanii walio kwenye chati kutodharau wachamga
Na Hamisi Magendela
INGAWA maeneo mbalimbali ya nchi yametoa wasanii wa muziki, ila uhalisia uliopo, Ilala ni sehemu mojawapo iliyo na inayoendelea kutoa wasanii wa kizazi kipya ambao wameweza kuitangaza vyema Wilaya hiyo na Tanzania kwa ujumla.
Mifano iko mingi ya wasanii ambao wameweza kuitangaza vyema Wilaya hiyo ikiwamo familia ya Kiba, Chidi Benz, Dully Sykes, Jahra Man, Akili ze Brain na wengineo wengi.
Pia, pia ukiachilia msanii mmoja-mmoja, yako makundi kadhaa ambayo yameweza kuitangaza vyema wilaya na kuifanya moja ya kitivo cha sanaa nchini.
Kundi la 'Dar Stamina' linaloongozwa na Abuu Sauti 'Shabaha' akiwa sanjari na Nurdin Biral 'Shetta', ni moja ya zao hilo.
Shetta ni miongoni mwa msanii ambao pia ni rais wa kundi hilo, mwenye mafaniko ya kuigwa kwa wasanii wachanga wanaoingia katika 'game' ya muziki huo na waliopo, ambao wanaonekana kujisahau licha ya kupata fursa ya kufanya shoo mbalimbali na kuwaingizia kipato.
Ni msanii aliyezaliwa jijini Dar es Salaam Julai 16, 1990 na kupata kuhitimu elimu yake ya msingi katika shule ya Ilala Boma mwaka 2008.
Nyota huyo anaevuma kwa sasa na wimbo wake 'Mdananda' ambao unafanya vizuri kwenye vituo mbalimbali vya redio na runinga, alianza kuingia kwenye tasnia ya muziki wa kizazi kipya tangu akiwa shule ya msingi Ilala Boma.
Alipata mshawasha wa kuingia katika fani hiyo baada ya kuvutiwa na mkongwe Joseph Haule 'Profesa Jay' wakati huo akijulikana na kwa jina la 'Nigger Jay' akiwa na kundi la Hard
Blasters.
"Nilivutiwa sana na Profesa Jay kutokana na uimbaji wake na jinsi anavyopangilia mashairi yake na anavyoweza kwenda na midundo, lakini pia Mwana FA, AY ni miongoni mwa wasanii wanaonipa msukumo wa kufanya vizuri kila siku ninapowasikiliza," anasema Shetta.
Wakati akiwa darasa la saba katika shule ya msingi Ilala Boma, aliachia wimbo wake wa kwanza ulioitwa Wadhifa, uliotengenezwa katika studio ya Dhahabu chini ya mtayarishaji
Pancho.
Anasema baada ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2004, alifanikiwa kuendelea na elimu ya sekondari ya Benjamini Mkapa hadi kidato cha nne, ambapo mwaka huo huo aliachia wimbo wake wa pili ulipewa jina la 'Nime-play' aliomshirikisha Mwana FA.
Wimbo huo ulimtambulisha vyema katika tasnia ya muziki huo na wadau wengi walitaka kujua safari yake ya muziki iko vipi.
Mkali huyo, anasema baada ya kuona wadau wengi wanahitaji kuona akifanya vyema, aliachia wimbo mwingine uliojulikana kwa jina la 'Nimechokwa' uliotengenezwa kwenye studio ya Mona Gangsta ikifuatiwa na wimbo mwingine ambao unafanya vyema kwa sasa katika vituo mbalimbali vya redio na luninga unaofahamika kwa jina la 'Mdananda'.
Anafafanua kuwa wimbo huo ulitengenezwa na Abdul Sykes 'Dully Sykes', na ukichanganywa na Pancho na kusema wimbo huo umekuwa gumzo katika jiji la Dar es Salaam na viunga
vyake.
Rais huyo wa kundi la Dar Stamina, anaweka wazi kuwa katika kufikia mafaniko aliyoyafikia kwa sasa kupitia muziki huo, alipata wakati mgumu wakati anaanza muziki kwa kukatishwa tamaa nawatayarishaji wa muziki kutokana na uchanga wake aliokuwanao wakati huo.
"Ukweli wengi walicheka, 'Maproducer' walinirudisha kila wakati na mmoja mkubwa katika tasnia ya muziki alitaka nimlipe dola 500 ili niweze kumshirikisha, hivyo inahitaji uvumilivu ili kufikia mafanikio," anasema Shetta.
Hivyo, anawaomba wasanii wachanga wajipange vizuri na kutokata tamaa mapema na changamoto wanazokutananazo katika harakati za muziki.
Anasema kutokana na uvumilivu wake, kwa sasa yupo katika hatua za mwisho za ujenzi wa nyumba yake maeneo ya Kimara Bucha.
Msanii huyo alizindua albamu yake ya kwanza Novemba 27 mwaka jana yenye nyimbo 10, iliyopewa jina la 'Simama kwa Stamina'.
Pia anawaomba wasanii walio kwenye chati kwa sasa kuacha kuwadharau wasanii wachanga kwani muziki unapanda na kushuka.
"Unaweza kumdharau msanii mchanga halafu baada ya kipindi kifupi anapanda kisanii na wewe ukashuka, hivyo ni vyema tukapendana na kupeana ushirikiano katika hali zote."
cioo
Thursday, February 9, 2012
New
Nurdin Biral 'Shetta'
Subscribe to:
Post Comments (Atom)





No comments:
Post a Comment