NA MWANDISHI WETU
RAIS Samia ametoa msamaha kwa taasisi za kidini zenye changamoto na kuielekeza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilifungulie Kanisa la Ufufuo na Uzima na taasisi nyingine za kidini, na kwamba lipewe miezi sita ya uangalizi katika kuzingatia miiko, masharti na sheria za uendeshwaji wake.
Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba, ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Rais Samia alipofanya ziara kuangalia miundombinu iliyoharibiwa na waandamanaji Agosti 29, mwaka huu.
“Waziri wa Mambo ya Ndani, baada ya hapa fuatilia utaratibu mzuri ziandikie upya taasisi za kidini, miiko yao na masharti ya uandikishaji na zile ambazo zilikuwa na shida ziweke kwenye uangalizi wa miezi sita, ipo taasisi ya Ufufuo na Uzima nenda kaifungulie. Ifungulie, wape masharti ya uangalizi ndani ya miezi sita. Ziandikie taasisi zote za kidini kuzikumbusha miiko na mipaka ya ufanyaji kazi, sawa sawa na sheria na Katiba ya nchi yetu,” amesema.
Sambamba na hilo, ameelekeza kurekebishwa kwa sharti linalotaka kufungiwa kwa nyumba ya ibada endapo atakosea kiongozi, akisisitiza kuwa anayekosea ndiye aadhibiwe bila kuathiri waumini kufanya ibada. “Akikosea Sheikh, usiadhibiwe msikiti na akikosea Askofu, wasinyimwe waumini kufanya ibada kwani ibada ni ushirika kati ya mwanadamu na Mungu wake na siyo yeye na askofu au sheikh,” amesema.





No comments:
Post a Comment