WAZIRI NDEJEMBI AWATAKA PBPA KUHAKIKISHA KUNAKUWEPO NA AKIBA YA KUTOSHA YA MAFUTA NCHINI - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Tuesday, November 25, 2025

WAZIRI NDEJEMBI AWATAKA PBPA KUHAKIKISHA KUNAKUWEPO NA AKIBA YA KUTOSHA YA MAFUTA NCHINI


NA MWANDISHI WETU 

WAZIRI wa Nishati, Deogratius Ndejembi amewataka Wakala wa Kuagiza Mafuta kwa Pamoja( PBPA) kuhakikisha kunakuwepo na akiba ya kutosha ya mafuta nchini lengo likiwa ni kuhakikisha uendelevu wa  shughuli za uzalishaji, usafirishaji na huduma nyingine muhimu ambazo zinategemea kwa kiasi kikubwa nishati hiyo 


Ndejembi ameyasema hayo Novemba 25,2025 Jijini Dar es salaam katika ofisi za PBPA ikiwa nimuendelezo wa ziara yake ya kuzungumza na viongozi wa Taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Nishati


Ametoa maelekezo kwa PBPA  kuhakikisha akiba ya mafuta hapa nchini inakuwa ya kutosha kwani itasaidia kuepuka uhaba wa ghafla unaoweza kusababisha ongezeko la gharama kwa wananchi na sekta binafsi na kukosekana kwa huduma hiyo.


 “Akiba ya mafuta ya kutosha kupitia uwekezaji katika vituo vya kuhifadhi kunaleta utulivu wa kiuchumi kwa Taifa kwani kunapokuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta, shughuli za uzalishaji, usafirishaji na biashara zinaendelea bila vizuizi na hii huongeza imani ya wawekezaji, hupunguza gharama za dharura, na hatimaye  kukuza ukuaji endelevu wa uchumi”.Amesisitiza Ndejembi


Aidha Ndejembi amewataka viongozi wa PBPA kuhakikisha wanawekeza zaidi katika kuimarisha miundombinu ya kupokelea mafuta  na kuhifadhia mafuta ili kuboresha usalama na ubora wa bidhaa kwa maslahi mapana ya Taifa 


Sambamba na hilo, Ndejembi amesisitiza wakala hao kushirikiana na wadau wa sekta binafsi kwenye mnyororo wa usambazaji mafuta lengo likiwa ni kuhakikisha upatikanaji wa maghala ya kuhifadhia mafuta ili kuondoa ucheleweshaji wa mafuta au upungufu usiotarajiwa. 


Awali akiwasilisha taarifa  ya utendaji kazi Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa kuagiza mafuta kwa pamoja, Erasto Simon ameeleza kuwa Katika kuhakikisha ufanisi katika utendaji kazi PBPA imejiandaa kuunganisha mifumo itakayosaidia kutoa bei linganifu kwenye bandari zote ili kuleta ufanisi katika usambazaji wa mafuta.


Katika ziara hiyo, Ndejembi ameambatana na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba pamoja na watalaamu wengine wa wizara.






No comments:

Post a Comment