TANESCO YAWATAKA WANANCHI KUTOFANYA SHUGHULI ZA KIUCHUMI KATIKA MIUNDOMBINU YA UMEME - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Saturday, May 16, 2026

TANESCO YAWATAKA WANANCHI KUTOFANYA SHUGHULI ZA KIUCHUMI KATIKA MIUNDOMBINU YA UMEME


NA MWANDISHI WETU 

WANANCHI wa mtaa wa wazo kata ya Tegeta jijijini Dar es Salaam wametakiwa kutojihusisha na shughuli za kibiashara katika maeneo ya miundombinu ya umeme ili kuepuka madhara mbalimbali yanayoweza kuwapata ikiwemo kupoteza maisha au kupata ulemavu.


Rai hiyo imetolewa  Mei 15, 2026 na Mhandisi wa  usafirishaji umeme Dar es salaam Philemon Tirukaizile kwa kushirikiana na Seikali ya Mtaa wa Wazo wakati wakitoa elimu kuhusu athari za kufanya shughuli au biashara kwenye miundombinu ya umeme hasa katika njia kubwa za kusafirisha umeme.


Akizungumza na wananchi wa eneo hilo Mwenyekiti wa Mtaa huo, Medard Mashauri amewataka wananchi hao kuelewa kuwa eneo walilopo ni hatarishi na ni mali ya TANESCO  hivyo hakuna sababu ya serikali kutumia nguvu kuwaondoa wananchi akiwasisitiza kuondoka wenyewe kwa hiari.


‘’Ni vyema wananchi ambao wameingia kwenye eneo la TANESCO  kuondoka  kwa hiari yao kwani serikali imeamua kuanza kutoa elimu kuhusu athari za kufanya biashara kwenye miundombinu ya umeme hivyo natoa rai muanze kuondoka wenyewe kabla ya hatua za kisheria’’ Alisema Bw. Mashauri.


Pia amewataka wananchi wasio waaminifu kuacha  tabia ya kuvunja au kuondoa alama zilizowekwa na TANESCO  kama marufuku ya kufanya shughuli katika eneo hilo kwani kufanya hivyo ni kuhujumu miundombinu ya serikali.


Kwa upande wake Mhandisi wa  usafirishaji umeme Dar es salaam Philemon Tirukaizile  amewataka wananchi wanaoishi Jirani na eneo hilo kutambua kuwa katika maeneo ambayo yanapitiwa na njia ya kusafirisha umeme mkubwa zinaathari katika maisha yao hivyo ametoa rai ya kuondoka na kutafuta maeneo mengine ambayo ni salama. 


‘’Eneo tulilopo hapa wakati laini inajengwa miaka ya nyuma kuliachwa mita 40 kutoka kwenye nguzo, kushoto 20 na kulia 20 wanaacha maeneo hayo ili kukulinda mwanadam  na miale inayopita kwenye hizo nguzo,pamoja na kujiepusha na hitilafu  za kudondokewa na Nyaya,’’alifafanua Mha. Philemon.


Nao baadhi ya wananchi wamekiri kuwa maeneo wanayofanyia biashara ni hatarishi hivyo wameiomba Serikali kuwatafutia maeneo ili kuondoka sehemu hiyo  ambayo ni maalumu kwa ajili ya miundombinu ya umeme.




No comments:

Post a Comment