NA MWANDISHI WETU
MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila, amesema ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) ni nyenzo muhimu katika kuleta mageuzi ya sekta ya afya nchini Tanzania.
Aidha imeelezwa kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kukidhi ongezeko la mahitaji ya huduma bora za afya na kupunguza mzigo wa kifedha kwa serikali.
Dhana hiyo imeelezwa wakati wa Kongamano la PPP kuhusu Mageuzi ya Sekta ya Afya chini ya FYDP IV na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 lilifanyika leo Juni 6 katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) jijini Dar es Salaam na kukutanisha wadau mbalimnali kama viongozi wa serikali, wataalamu wa afya na wawekezaji kujadili fursa za kupanua ushirikiano wa PPP katika sekta ya afya.
Kafulila, amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuimarisha huduma za afya kwa miaka ya hivi karibuni, ikiwemo uwekezaji uliowezesha baadhi ya matibabu maalumu yaliyokuwa yakifanyika nje ya nchi kupatikana ndani ya Tanzania.
Amesema kuwa ongezeko la idadi ya watu, kuongezeka kwa umri wa kuishi pamoja na mahitaji makubwa ya huduma za afya za kibingwa vinaifanya serikali kushindwa kugharamia mahitaji yote ya sekta hiyo kwa kutumia mapato ya kodi na mikopo pekee.
Kafulila amesema PPP ni fursa muhimu ya kuhamasisha rasilimali za ziada kwa ajili ya miundombinu ya afya, vifaa tiba na usimamizi wa huduma huku wananchi wakiendelea kupata huduma bora.
“Uchumi wetu unaendelea kukua na mahitaji ya huduma za afya yanaendelea kuongezeka. Uwezo wa serikali kugharamia huduma zote hizi kwa kutumia kodi na mikopo una mipaka,” amesema Kafulila.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano huo akisema wadau wanapaswa kubaini maeneo ambayo sekta binafsi inaweza kuleta ubunifu na kuboresha huduma ambazo bado hazipatikani au zinazotolewa kwa kiwango kisichoridhisha.
Aliwahimiza wawekezaji na wataalamu wa afya kuangalia mifano ya mafanikio kutoka mataifa mengine na kuona namna inavyoweza kutumika katika mfumo wa afya wa Tanzania.
Dk Nkoronko amesema kuna haja ya kutafuta fursa za kuanzisha huduma za kibingwa, teknolojia za kisasa za tiba na suluhisho bunifu kupitia mifumo ya ushirikiano.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Hospitali Binafsi vya Afya Tanzania (APHFTA), Dk Mahmood Mringo, amesema PPP haipaswi kutazamwa kama uhamishaji wa mtaji kutoka sekta binafsi kwenda sekta ya umma pekee, bali kama njia ya kuhamasisha rasilimali zote zilizopo kwa ajili ya kuboresha ustawi wa wananchi.
Amesema afya na elimu ni huduma muhimu za msingi zinazohitaji mifumo endelevu ya ufadhili na ubia wa kibunifu ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka.
Dk Mringo alibainisha kuwa wananchi huchangia maendeleo ya taifa kupitia kodi na hivyo wanatarajia kupata huduma bora za afya.








No comments:
Post a Comment