BODI YA USHAURI YA TARURA YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA DMDP II NA CERC KIGAMBONI ‎ - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Thursday, July 30, 2026

BODI YA USHAURI YA TARURA YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA DMDP II NA CERC KIGAMBONI ‎


NA MWANDISHI WETU


Bodi ya Ushauri ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeridhishwa na kasi na ubora wa utekelezaji wa miradi ya DMDP II na CERC inayotekelezwa katika wilaya ya Kigamboni huku ikimtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuongeza kasi ya ujenzi ili kuhakikisha kazi zinakamilika kwa wakati uliopangwa.

‎Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya miradi katika maeneo ya Mwasonga, Geza Ulole, Fullshangwe na Kibada, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TARURA, Mhandisi Florian Kabaka amesema miradi mingi inaendelea kwa kasi ya kuridhisha, ubora unaokidhi viwango na ipo ndani ya ratiba ya utekelezaji.

‎Hata hivyo, amebainisha kuwa mradi mmoja umechelewa kulinganisha na ratiba iliyopangwa na kusisitiza kuwa Mkandarasi husika anapaswa kuongeza rasilimali ikiwemo nguvu kazi na vifaa ili kufidia muda uliopotea na kukamilisha mradi kwa wakati.

‎"Ni muhimu kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati hususan ile yenye mchango mkubwa katika maandalizi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON). Hakuna sababu ya kuchelewesha miradi yenye manufaa makubwa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla", amesema Mhandisi Kabaka.

‎Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff amesema Wakala utaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha maagizo ya Bodi ya Ushauri yanazingatiwa kikamilifu.

‎"Tumeridhishwa na kasi na ubora wa utekelezaji wa miradi hii, hata hivyo kwa mkandarasi aliyebaki nyuma kidogo tutaendelea kumsimamia kwa karibu ili aharakishe utekelezaji kwani TARURA haitasita kuchukua hatua za kimkataba endapo masharti ya mkataba hayatatekelezwa", amesema Mhandisi Seff.

‎Aidha, viongozi hao waliwahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kulinda miundombinu inayojengwa, kutoa ushirikiano katika maeneo yanayohitaji kupisha ujenzi na kuendelea kufuata taratibu zinazohusu fidia ambazo zinaendelea kushughulikiwa.

‎Naye, Meneja wa TARURA mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Godfrey Mkinga amesema miradi minne ya DMDP II inayotekelezwa katika wilaya ya Kigamboni ina thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 20.1 na itahusisha ujenzi wa kilomita 43.26 za barabara kwa kiwango cha lami.

‎Amesema baadhi ya miradi hiyo imefikia zaidi ya asilimia 80 ya utekelezaji huku mingine ikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi na inatarajiwa kukamilika kwa awamu kuanzia Oktoba 2026 hadi Aprili 2027.

‎Mkinga ameongeza kuwa changamoto zilizojitokeza zikiwemo uhamishaji wa miundombinu ya huduma na malipo ya fidia kwa baadhi ya wananchi zinaendelea kutatuliwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali bila kuathiri maendeleo ya utekelezaji wa miradi.

‎Kwa nyakati tofauti wananchi wa maeneo yanayopitiwa na miradi hiyo wameipongeza serikali kupitia TARURA kwa kuendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya barabara wakisema miradi hiyo itaondoa adha ya usafiri wakati wa mvua, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma, kuongeza usalama wa watumiaji wa barabara pamoja na kufungua fursa mpya za biashara na ukuaji wa uchumi wa wilaya ya Kigamboni.





No comments:

Post a Comment