NA MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imemkamata Mtumishi wa Hospitali ya Ocean Road, Goodluck Nyakaselula (35) kwa tuhuma za kusafirisha Dawa za Kulevya aina ya bangi kilogramu 106. 04.
Imeelezwa kuwa Nyakaselula (35), mkazi wa Mbezi Beach, Dar es Salaam, alikamatwa jijini Arusha akitokea nchini Kenya akiwa na dawa hizo ambako alikuwa akisomea utaalamu wa picha (Radiographer).
Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lymo, ameibainisha hayo leo jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa Nyakaselula alikamatwa akiwa kwenye gari aina ya Toyota Premio lenye namba za usajili T 853 ECX.
Pia Kamishna amesema kwamba mtuhumiwa huyo amekamatwa kwenye oparesheni iliyofanyika Mei na Juni mwaka huu ambapo jumla ya watu 188 walikamatwa na taratibu zinaendelea kuwafikisha mahakamani.
Aidha ameongeza kwamba katika maeneo mbalimbali walifanikiwa kukamata tani 22.6 za dawa za kulevya, lita 30.5 na kilogramu 19.94 za dawa tiba zenye asili ya kulevya na iliteketeza ekari 228.5 za mashamba ya bangi pamoja na tani 3.3 za bangi na mirungi.
Pia ilikamata magari sita, bajaji mbili na pikipiki 33 zilizohushwa na uhalifu huo pia jijini Dar es Salaam zilikamatwa kilogramu 19.94 za bidhaa zilizotambulishwa kama virutubisho vya lishe aina ya AFA CELL (Moringa Extract) katika eneo la mizigo inayosafirishwa kwenda nje ya nchi kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
"Baada ya kufanyiwa uchunguzi wa maabara, ilibainika kuwa bidhaa hizo zilikuwa na kiambata cha dawa tiba yenye asili ya kulevya aina ya Prazepam.
Pia katika operesheni iliyofanyika eneo la ukaguzi wa mizigo la Bandari ndogo ya boti zinazotoa huduma kati ya Dar es Salaamı na Zanzibar, zilikamatwa gramu 972.05 za mirungi zilizokuwa zikisafirishwa na mtuhumiwa Kalsam Abdurahman Sebbi (43), raia wa Kenya mwenye makazi yake Mombasa, wilayani Kigamboni zilikamatwa gramu 162.48 za heroin zilizomuhusisha mtuhumiwa Omary Miraji Mbonaeni.
Aidha, wilayani Same mkoani Kilimanjaro, eneo la kituo cha mabasi yaendayo mikoani, zilikamatwa kilogramu 240 za mirungi zikiwa zimefichwa ndani ya mabegi ya nguo. Katika tukio hilo, walikamatwa watuhumiwa Irene Obedi Sule na Eliasi Obedi Sule," amesema
Ameongeza kuwa kwa operesheni zilizofanyika katika mikoa mingine nchini, zilikamatwa tani 19.5 za bangi, tani 2.6 za mirungi, gramu 11.63 za heroin na kilogramu 40 za skanka.
Aidha, tani 3.3 za bangi na mirungi pamoja na ekari 228.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa katika wilaya za Chamwino mkoa wa Dodoma, kijiji cha Mwengei kilichopo wilaya ya Kilwa mkoa wa Lindi na katika vijiji vya Busekeseke na Miembeni vilivyopo wilaya ya Sengerema na Geita.
Pia natoa wito kwa Wafanyakazi wa mashirika ya Umma kuhakikisha wanakuwa waaminini na wasijiingize kwenye mitego ya kufanya biashara ya dawa za Kulevya, kwani sheria ni msumeno itamfikia kila atakayeingia kwenye biashara hiyo haramu.












No comments:
Post a Comment