Mollel awaita wazazi na wanafunzi Four Points by Sheraton na Rock City Mall - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Monday, July 27, 2026

Mollel awaita wazazi na wanafunzi Four Points by Sheraton na Rock City Mall

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

GLOBAL Education Link (GEL) imesema jumla ya wanafunzi, wazazi na walezi 1,113 wamefikiwa na kupatiwa huduma kupitia maonesho ya Global Education Fair 2026 yaliyofanyika Zanzibar, Dodoma na Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kukamilika kwa maonesho yaliyofanyika Julai 25, 2026 katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa GEL, Abdulmalik Mollel, alisema mwitikio huo unaonesha kuongezeka kwa uhitaji wa taarifa sahihi kuhusu fursa za kusoma nje ya nchi.

Alisema kupitia maonesho hayo, washiriki walipata ushauri kuhusu uchaguzi wa kozi, vyuo vikuu, scholarships, gharama za masomo, malazi, visa na maisha ya mwanafunzi katika mataifa mbalimbali.

“Mwitikio tulioupata Zanzibar, Dodoma na Dar es Salaam unaonesha kuwa wanafunzi na wazazi wanahitaji mwongozo sahihi kabla ya kufanya maamuzi kuhusu elimu ya juu,” alisema Bwana Mollel.

Alisema zaidi ya watu 700 walitembelea banda la GEL katika maonesho yaliyofanyika Viwanja vya Maisara, Zanzibar, watu 168 walihudhuria maonesho ya Dodoma na wengine 245 walishiriki maonesho ya Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Mollel, jumla ya maombi 209 ya udahili yaliwasilishwa kupitia maonesho hayo matatu.

Alisema Zanzibar ilipokea maombi 79 ya udahili katika vyuo vikuu vya China, India, Malaysia, Afrika Kusini na mataifa mengine, ambapo wanafunzi 30 walipata udahili papo kwa papo.

Kwa upande wa Dodoma, maombi 78 yaliwasilishwa, wanafunzi 50 wakapata udahili papo kwa hapo na wengine 40 wakafungua mafaili mapya kwa ajili ya kuendelea na taratibu za kujiunga na vyuo.

Katika maonesho ya Dar es Salaam, watu 108 walionesha nia ya kuendelea na taratibu za udahili, maombi 52 yaliwasilishwa, barua 41 za udahili zilikuwa tayari na mafaili mapya 15 yalifunguliwa.

Alisema mafanikio hayo yametokana na kuwapa wanafunzi nafasi ya kukutana moja kwa moja na wawakilishi wa vyuo vikuu, kuuliza maswali na kupata ushauri unaozingatia matokeo yao ya kitaaluma, uwezo wa kifedha na malengo ya baadaye.

Mollel alisema Global Education Fair hailengi kuwasaidia wanafunzi kupata udahili pekee, bali pia kuwajengea uwezo wa kuchagua taaluma zenye fursa katika soko la ajira na zinazoweza kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Tunataka mwanafunzi achague kozi inayolingana na uwezo wake, mahitaji ya soko la ajira na mchango anaoweza kuutoa katika maendeleo ya Taifa, badala ya kuchagua kwa kufuata mkumbo,” alisema.

Alitaja baadhi ya maeneo yenye fursa kuwa ni sayansi za afya na tiba, uhandisi, teknolojia ya habari na mawasiliano, akili bandia, sayansi ya data, usalama wa mtandao, nishati, kilimo cha kisasa, biashara, fedha, usafirishaji, utalii, elimu na teknolojia za viwanda.

Katika maonesho ya Dar es Salaam, vyuo vilivyoshiriki ni pamoja na Lovely Professional University, Sharda University, SRM University–AP, Maharishi Markandeshwar (Deemed to be University)—MMU, Noida International University na Asia Pacific University of Technology and Innovation.

Pia kulikuwa na mabanda yaliyotoa taarifa kuhusu fursa za kusoma China, Malaysia, North Cyprus, Marekani, Canada, Uingereza, Uholanzi, Australia, Ireland, New Zealand na Dubai.

Mollel aliwaalika wakazi wa Kanda ya Kaskazini kushiriki maonesho yatakayofanyika Julai 28, 2026 katika Hoteli ya Four Points by Sheraton jijini Arusha.

Aidha, aliwaalika wakazi wa Kanda ya Ziwa kufika kwenye maonesho yatakayofanyika Julai 30, 2026 katika Rock City Mall jijini Mwanza, kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni.

Aliwataka wanafunzi waliomaliza Kidato cha Nne, Kidato cha Sita, stashahada, shahada na wale wanaotafuta nafasi za masomo ya uzamili kufika wakiwa na matokeo au vyeti vyao.

“Tunawaalika wanafunzi, wazazi na walezi wa Arusha, Mwanza na mikoa ya jirani kufika na kupata ushauri wa moja kwa moja kuhusu kozi, vyuo, udahili na scholarships,” alisema Mollel.

Alisema GEL itaendelea kuwaongoza wanafunzi kuanzia hatua ya kuchagua kozi na chuo, kuomba udahili, kupata visa na malazi hadi maandalizi ya safari ya kwenda kusoma nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment