WATANZANIA KUNUFAIKA NA UMEME WA UHAKIKA; MRADI WA CHALINZE–DODOMA WAFIKIA ASILIMIA 89 YA UTEKELEZAJI - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Wednesday, July 1, 2026

WATANZANIA KUNUFAIKA NA UMEME WA UHAKIKA; MRADI WA CHALINZE–DODOMA WAFIKIA ASILIMIA 89 YA UTEKELEZAJI


NA MWANDISHI WETU, MOROGORO


Watanzania katika maeneo mbalimbali nchini wanatarajiwa kunufaika na huduma ya umeme yenye uhakika zaidi kutokana na maendeleo makubwa ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma, ambayo sasa imefikia asilimia 89 ya utekelezaji.


Mradi huo wenye urefu wa kilometa 345 unatarajiwa kukamilika Agosti 21, 2026 na utaongeza uwezo wa kusafirisha umeme kutoka vyanzo vikubwa vya uzalishaji kwenda maeneo yenye mahitaji makubwa ya nishati, hatua itakayochochea maendeleo ya kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi.


Akikagua maendeleo ya mradi huo Julai 1, 2026, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb), amesema mradi huo ni uwekezaji muhimu unaolenga kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika kwa matumizi ya nyumbani, biashara ndogo na kubwa, pamoja na shughuli za uzalishaji.


Amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuimarisha Gridi ya Taifa na kuwezesha umeme unaozalishwa katika Kituo cha Kufua Umeme cha Julius Nyerere chenye uwezo wa megawati 2,115 kuwafikia wananchi na sekta mbalimbali za uchumi kwa ufanisi zaidi.


“Umeme wa uhakika una maana ya maisha bora zaidi kwa wananchi, biashara kukua, viwanda kufanya kazi bila kukatika kwa huduma na huduma za kijamii kama hospitali na shule kuendelea kutoa huduma kwa ufanisi,” amesema Mhe. Ndejembi.


Aidha, amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika miradi ya umeme ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata huduma ya nishati inayowawezesha kuongeza kipato na kuboresha ustawi wao.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema ongezeko la uwekezaji katika miundombinu ya umeme limechangia kuongezeka kwa kasi ya uunganishaji wa wateja wapya, jambo linaloonesha namna umeme unavyoendelea kuwa sehemu muhimu ya maisha na maendeleo ya wananchi.


Amesema katika mwaka wa fedha 2025/26, TANESCO imeweka rekodi mpya kwa kuunganisha zaidi ya wateja laki nane, idadi ambayo haijawahi kufikiwa tangu Tanzania ipate uhuru.


“Kila mteja mpya anayepata umeme ni fursa mpya ya biashara, elimu bora kwa watoto, huduma bora za afya na ongezeko la kipato kwa familia. Hii ndiyo maana ya uwekezaji huu mkubwa wa Serikali katika sekta ya umeme,” amesemaTwange.


Awali, Meneja wa Mradi, Mha. Newton Mwakifamba, amesema kazi zinaendelea vizuri na zinatarajiwa kukamilika Agosti 21, 2026 kwa mujibu wa ratiba ya mkataba, na hivyo kufungua ukurasa mpya wa upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa Watanzania wengi zaidi.






No comments:

Post a Comment