KATAMBI: MAHAKAMA PEKEE NDIYO YENYE MAMLAKA YA KUTOA TAFSIRI YA KATIBA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Thursday, July 2, 2026

KATAMBI: MAHAKAMA PEKEE NDIYO YENYE MAMLAKA YA KUTOA TAFSIRI YA KATIBA


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amesema ulinzi na usalama wa Tanzania ni wajibu wa kila mwananchi, akisisitiza kuwa kila Mtanzania anatakiwa kushiriki katika kulinda amani, umoja wa kitaifa na mali za umma kwa kuzingatia Katiba na sheria za nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Julai 2, 2026, Katambi alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuzuia uhalifu kabla haujatokea kwa kubaini viashiria, mianya, tabia na mipango inayoweza kusababisha vitendo vya uhalifu, ili kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao unaendelea kuimarika.

Aliwataka wananchi kuheshimu sheria za nchi na kutumia taratibu za kisheria wanapoamini haki zao zimekiukwa, badala ya kujichukulia mamlaka, akisema hatua hiyo ndiyo njia sahihi ya kulinda utawala wa sheria na amani nchini.

Katambi alisema kumekuwa na upotoshaji kuhusu haki ya kukusanyika na kushirikiana na wengine, akieleza kuwa ingawa haki hiyo imetambuliwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, utekelezaji wake unapaswa kufuata masharti yaliyowekwa na sheria.

Alisema Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ndiyo yenye dhamana ya kuhakikisha usalama wa ndani ya nchi, hivyo ina wajibu wa kubaini mapema viashiria vya uhalifu na kuchukua hatua za kuzuia madhara kabla hayajatokea.

Aidha, alisema hoja kuhusu kuwepo au kutokuwepo kwa uvunjifu wa Katiba haiwezi kutolewa uamuzi na mtu au taasisi yoyote isipokuwa Mahakama, akisisitiza kuwa mamlaka hayo yameainishwa katika Ibara ya 107A(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katambi alifafanua kuwa uhuru wa kushirikiana na wengine, kufanya mikutano ya hadhara na maandamano si haki isiyo na mipaka, bali utekelezaji wake unapaswa kuzingatia sheria zinazolenga kulinda usalama wa umma, amani, afya ya jamii pamoja na haki na uhuru wa wengine.

Alisema Ibara ya 20(1) ya Katiba ndiyo msingi wa haki ya kukutana, kukusanyika kwa amani, kuandamana na kushiriki mikutano ya umma, lakini haki hiyo inapaswa kutekelezwa kwa mujibu wa sheria zilizopo.

Pia alisema Katiba imeweka wazi kuwa kila raia ana wajibu wa kulinda uhuru, mamlaka, ardhi na umoja wa taifa pamoja na kuheshimu mali za umma na za watu binafsi, akisisitiza kuwa jukumu hilo ni la kila Mtanzania.

Katambi aliongeza kuwa Kifungu cha 42 cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi, Sura ya 322, kinatoa mamlaka kwa Jeshi la Polisi kusimamia na kuratibu mikusanyiko na maandamano kwa kuelekeza muda na njia zitakazotumika ili kuhakikisha usalama, utulivu wa umma na ulinzi wa watu pamoja na mali zao.

No comments:

Post a Comment