NA MWANDISHI WETU, DODOMA
MKUU wa chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI),Profesa Tumaini Gurumo, amesema Tanzania inahitaji kuongeza idadi ya wataalamu wa usafirishaji na usimamizi wa mnyororo wa bidhaa ili kuongeza tija, ushindani wa bidhaa za ndani na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Profesa Gurumo,amebaisha hayo jana jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya 49 ya Nanenane kwenye viwanja vya Dkt John Malecela.
Aidha,amesema kuwa chuo hicho kunasifika kwa kutoa mafunzo yanayohusiana na masuala ya bahari na mabaharia, kinatoa pia mafunzo ya lojistiki na usimamizi wa mnyororo wa usambazaji wa bidhaa, eneo ambalo ni muhimu katika kukuza biashara nchini.
Mtaalamu huyo ,amesema kilimo na shughuli za bahari haziwezi kutenganishwa kwa kuwa mazao yanayozalishwa nchini yanahitaji mifumo bora ya usafirishaji ili kuwafikia walaji na masoko kwa wakati.
Hata hivyo, Profesa Gurumo, amesema uwepo wa wataalamu wenye ujuzi katika mnyororo wa usafirishaji ni sehemu ya maandalizi ya Tanzania kushindana katika masoko ya kimataifa, na ushindani wa kiuchumi hauishii ndani ya mipaka ya nchi.
Akizungumzia kuhusu Akili Unde, Profesa Gurumo amesema DMI imeendelea kuboresha mitaala yake ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia, ikiwemo matumizi ya mifumo ya kidijitali na akili bandia (AI) katika sekta ya usafirishaji.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wahitimu wanaingia katika soko la ajira wakiwa na ujuzi unaoendana na mahitaji ya sasa ya sekta ya usafirishaji na uchumi kwa ujumla.






No comments:
Post a Comment