JUKWAA la Wanawake Vijijini Tanzania (RWA Tanzania limeainisha maeneo yatakayoimarisha sauti, uongozi na ushiriki wao katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kimazingira.
Hayo yamesemwa na Mwanajukwaa wa RWA Tanzania, Judith Singibala wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii, katika Viwanja vya Nanenane Nzuguni mkoani Dodoma.
Amesema jukwaa hilo lililo anzishwa mwaka 2023 ni mtandao wa wanawake wa vijijini na limeendelea kukua kwa kasi, likiwa na wanachama 2,473 waliopo katika mikoa mbalimbali nchini wanaolenga kuimarisha sauti, uongozi na ushiriki katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kimazingira.
"Jukwaa linawaunganisha wanawake wadogo wakulima, wafugaji, wavuvi, wahifadhi wa mbegu za asili na wengine wanaotegemea rasilimali za asili kwa maisha yao na matokeo yamekuwa mazuri kwao," amesema.
Mwanajukwaa huyo ametaja ambayo
RWA Tanzania inatekeleza kwa waledi ni kilimo cha kiikolojia ambapo wamekuwa wakielimisha na kuhamasisha matumizi ya mbinu za kilimo kisichotumia kemikali au sumu zinazoharibu udongo na mazingira.
Kufundisha mbinu za utengenezaji wa mbolea za asili na viuatilifu vya kibaolojia ili kupunguza gharama za uzalishaji kwa mkulima mdogo na kukuza ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi kupitia hifadhi ya udongo na uvunaji wa maji.
Alitaja eneo lingine ambalo wanawake hao wanafanya ni kuanzisha kuanzisha na kusimamia benki za mbegu katika ngazi ya jamii ili kulinda na kuhifadhi kiasili zinazoelekea kutoweka.
"Kuendesha na kuendeleza mfumo wa Ubadilishanaji wa Mbegu kati ya wakulima wa ndani na wanajukwaa wa kikanda kama vile ushirikiano wetu na wanajukwaa kutoka nchi za Madagascar, Zambia, Lesotho, na Zimbabwe," amesema.
Poa wanatetea uhuru wa mbegu, ili kuondoa utegemezi wa mbegu za viwandani na kurudisha umiliki wa mbegu mikononi mwa wakulima.
"Tunaelimisha jamii kuhusu haki za wanawake za kurithi, kumiliki, na kutumia ardhi kwa ajili ya uzalishaji, kujenga uwezo wa wanawake vijijini kushiriki kikamilifu katika vyombo vya maamuzi kuanzia ngazi ya kijiji hadi kitaifa na kupinga mifumo ya mfumo-dume na ukatili wa kiuchumi unaorudisha nyuma maendeleo ya mwanamke mlimaji," amesema.
Singibala ametaja aneo linginw ni kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi hasa katika kuhamasisha wanawake vijijini kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabia ya nchi, ikiwa ni pamoja na kampuni endelevu za upandaji miti kwa ajili ya mustakabali wa kijani.
Pia, alisema wanashughulikia maswala ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake ikiwa ni pamoja na imani potofu ,upatikanaji usio sawa wa rasilimali na tofauti za kiuchumi.
Amesema RWA Tanzania ni sehemu ya mtandao wa Rural Women’s Assembly unaofanya kazi katika nchi mbalimbali za Afrika kwa lengo la kujenga mshikamano wa wanawake wa vijijini na kutetea haki zao.







No comments:
Post a Comment