NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imetoa muda wa miezi sita kwa wamiliki na waendeshaji wa miundombinu muhimu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nchini kujisajili kupitia mfumo maalumu wa CII Portal, hatua inayolenga kuhakikisha miundombinu hiyo inapata ulinzi wa kisheria.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amesema usajili huo unatekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao Na. 14 ya mwaka 2015 pamoja na Tangazo la Serikali Na. 147 la Juni 19, 2026.
Amesema kipindi cha usajili kilianza Juni 19, 2026 na kinatarajiwa kukamilika Desemba 19, 2026, hivyo kuwataka wamiliki na waendeshaji wa miundombinu hiyo kutumia muda uliowekwa kukamilisha usajili.
Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari leo, Agosti 19, 2026, jijini Dar es Salaam, Waziri Kairuki amesema Serikali imebainisha miundombinu muhimu ya TEHAMA kutoka sekta mbalimbali za umma na binafsi Tanzania Bara na Zanzibar ambayo inapaswa kusajiliwa na kulindwa.
Amesema miundombinu hiyo inahusisha mali, vifaa, mifumo ya kompyuta na mitandao yenye umuhimu mkubwa kwa usalama, uchumi na ustawi wa jamii, ambapo kutofanya kazi kwake kunaweza kusababisha athari kubwa nchini.
Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, sekta zenye miundombinu muhimu ya TEHAMA ni pamoja na Habari na Mawasiliano, Fedha na Benki, Maji, Afya, Nishati, Madini, Usafirishaji, Chakula na Kilimo, Ujenzi, Uchumi wa Buluu, Mazingira, Viwanda, Ulinzi, Anga, Elimu, Utawala wa Kiraia, Ulinzi wa Raia, Ardhi pamoja na Usalama na Utulivu wa Umma.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha miundombinu hiyo inaendelea kuwa salama, inapatikana na kufanya kazi kwa uhakika hata wakati wa mashambulizi ya mtandao, hitilafu za kiufundi au majanga.
Waziri Kairuki amesema Serikali pia imeandaa miongozo mitano itakayowawezesha wamiliki na waendeshaji kutambua, kusimamia na kulinda miundombinu muhimu ya TEHAMA.
Miongozo hiyo ni Mwongozo wa Utambuzi na Usimamizi wa Miundombinu Muhimu ya TEHAMA, Mwongozo wa Ukaguzi wa Miundombinu Muhimu ya TEHAMA, Mwongozo wa Tathmini ya Hatari, Mwongozo wa Uadilifu na Uhalisia wa Data pamoja na Mwongozo wa Mipango ya Urejeshaji wa Huduma Baada ya Janga.
Aidha, amesema wamiliki na waendeshaji wa miundombinu hiyo wanapaswa kufungua akaunti kupitia CII Portal kabla ya kuanza kuwasilisha taarifa za miundombinu yao.
Ametoa wito kwa wadau wenye changamoto katika mchakato wa usajili au masuala ya kiusalama kushirikiana na wataalamu wa Wizara kupitia dawati la msaada.
Ametaja namba za msaada kuwa 0612 600 600, 0612 400 400 na 0733 124 972, pamoja na barua pepe supportcii-registry@mawasiliano.go.tz na fomu ya maulizo inayopatikana kupitia CII Portal.
Waziri Kairuki pia amesisitiza kuwa matukio ya kiusalama yanayohusisha miundombinu muhimu ya TEHAMA yanapaswa kuripotiwa kwa mamlaka husika ndani ya saa 24 tangu kubainika kwake.
Amesema taarifa hizo zitasaidia mamlaka kufahamu tukio lililotokea, aina ya athari iliyosababishwa au inayoweza kutokea, huduma zilizoathirika au zinazoweza kuathirika pamoja na hatua za awali zilizochukuliwa na mmiliki au mwendeshaji.
Sambamba na hayo, Waziri Kairuki amesema Serikali imeweka adhabu kali kwa mtu atakayebainika kuharibu miundombinu muhimu ya TEHAMA.
Amesema kwa mujibu wa Kifungu cha 29 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, mtu anayehusika anaweza kutozwa faini isiyopungua Sh milioni 100 au mara tatu ya hasara iliyosababishwa, au kifungo kisichopungua miaka mitano, au adhabu zote kwa pamoja.
Amesema ulinzi wa miundombinu hiyo ni muhimu kutokana na uwezekano wa uharibifu wake kusababisha madhara makubwa kiusalama, kiuchumi na kijamii.
Waziri Kairuki amewataka taasisi, mashirika na wadau wote wanaomiliki au kuendesha miundombinu muhimu ya TEHAMA kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi na kwa wakati, huku wakizingatia matakwa ya sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa.
Amesema mafanikio ya zoezi hilo yanategemea ushirikiano, uwajibikaji na dhamira ya pamoja kati ya Serikali, sekta binafsi na wananchi katika kulinda miundombinu muhimu ya TEHAMA nchini.







No comments:
Post a Comment