KATIKA kuhakikisha Dira ya maendeleo 2050 inafikiwa kikamilifu,Shirika lisilo la kiserikali la INADES-Formation Tanzania limesema linaendelea kutekeleza kauli mbiu ya Maonesho ya Kilimo Nanenane Kitaifa ya mwaka 2026 ya "Tambua Soko, Ongeza Tija, Tekeleza Dira ya Taifa 2050" ikiwemo kuwawezesha wakulima na wafugaji kupata elimu ya kifedha,na kuchangia kuongeza uzalishaji, kuwaunganisha na masoko ya ndani na nje ya nchi kupitia bidhaa wanazozalisha.
Hayo yamebainishwa leo mapema Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa INADES-Formation Tanzania, Jacqueline Nicodemus,wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati wa Maonesho ya Kilimo Nanenane Kitaifa yanayoendelea Jijini Dodoma, katika viwanja vya Dkt John Malecela.
Aidha,Bi Jacqueline amesema shirika hilo limejikita katika kuhamasisha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira kwenye sekta za kilimo na ufugaji ili kuongeza tija na kuboresha maisha ya wananchi.
Mkurugenzi huyo amesema shirika hilo linalenga kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa jamii ya wakulima na wafugaji kwa kuwajengea uwezo wa kuzalisha kwa ufanisi, pamoja na kuongeza thamani ya mazao na mifugo pamoja na kuwaunganisha na fursa mbalimbali za masoko.
Sanjari na hayo Bi Jacqueline amesema kwa sasa wamepanua wigo wa shughuli zao kwa kuhakikisha mkulima haishii kwenye uzalishaji wa mazao pekee, bali pia anashiriki katika shughuli za ufugaji ili kuongeza vyanzo vya kipato, ameongeza kuwa wanatoa mafunzo kwa njia ya masafa pamoja na vitabu na machapisho mbalimbali vinavyowasaidia wakulima na wafugaji kujifunza mbinu bora za uzalishaji na ufugaji wenye tija.
Vilevile amesema katika utekelezaji wa shughuli zake, INADES-Formation Tanzania imeendelea kuwekeza katika maeneo ya kilimo, ufugaji, hifadhi ya mazingira pamoja na kufungua fursa za kiuchumi katika wilaya, mikoa na vijiji mbalimbali kwa kushirikiana na mamlaka husika nchini.
Jacqueline amebainisha kuwa kwa sasa INADES inafanya kazi katika mikoa ya Dodoma, Singida na Iringa, likihudumia jumla ya vijiji 26 na kuwafikia zaidi ya wananchi 150,000 kupitia vikundi vya wakulima, taasisi mbalimbali pamoja na wakulima mmoja mmoja.
Amesema ushiriki wa INADES-Formation Tanzania katika Maonesho ya Kilimo Nanenane unalenga kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kilimo endelevu, ufugaji wenye tija, uhifadhi wa mazingira na matumizi ya teknolojia zinazoongeza uzalishaji huku zikiimarisha fursa za kiuchumi kwa jamii.





No comments:
Post a Comment