NA MWANDISHI WETU
ZAIDI ya shilingi bilioni 3 zinatarajiwa kutumiwa na Shirika la Island of Peace (IDP), kutekekeza miradi mitatu mpya ya Kilimo Endelevu Arusha+ II, ECO-FOOD II na SAFI, kwa lengo la kuendeleza kilimo ikolojia na lishe bora.
Miradi hiyo mipya ambayo itatekelezwa kwa miaka miwili na mitatu ni mwendelezo wa mafanikio ya miradi ya Kilimo Endelevu Arusha+ na ECO-FOOD ambayo imemalizika.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa IDP, Ayesiga Buberwa wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya hafla ya uzinduzi wa miradi hiyo mipya ambayo imefadhiliwa na mashirika kutoka nchini Ubelgiji na Luxembourg
"Bajeti ya jumla ya miradi yote mitatu ni takribani Euro milioni 1.3, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 3 za Kitanzania na kila mradi una bajeti yake binafsi," amesema.
Amesisitiza kuwa zaidi ya asilimia 90 ya bajeti hiyo inaenda moja kwa moja chini kwa walengwa kupitia mafunzo, uanzishaji wa viwanda vidogo na vifaa vya usambazaji wa vyakula mijini.
Ayesiga amesema mradi uliopita umetimiza malengo kwa zaidi ya asilimia 85, hivyo ujio wa mradi mpya unaenda kukamilisha eneo lilobakia.
"Tumetimiza zaidi ya asilimia 85 ya malengo ya mradi uliopita, lakini mifumo ya chakula ni jumuishi na ina changamoto nyingi. Miradi hii mipya inakuja kutatua changamoto tulizozibaini na kuendeleza bunifu nzuri tulizozijifunza," amefafanua
Mkurugenzi huyo Mradi ECO-FOOD utajikita katika kuwaongeza na kuwajengea uwezo wajasiriamali wa kilimo ikolojia katika usindikaji, uongezaji thamani na uuzaji, ili walaji wapate mazao kwa urahisi.
"Kwa awamu hii, wakulima angalau 500 kupitia wakulima vichocheo ambao wataeneza elimu. Kwa upande wa wajasiriamali, wataendelea na wajasiriamali 50 wa Arusha DC waliopo na kuongeza vikundi vipya vitano hadi 10 vya vijana wabunifu, kama wale wanaotaka kuzalisha mbolea kutokana na taka za masokoni," amesema
Kuhusu Mradi wa SAFI unalenga kutatua changamoto ya upatikanaji wa pembejeo hai. Utahakikisha wakulima wanapata mbolea za asili, viuatilifu hai na zana ndogo za kisasa.
"Kilimo ikolojia kinahitaji nguvu. Kutwanga pilipili na kuchanganya na majani kutengeneza dawa ni kazi ngumu, hasa kwa wanawake. Tunataka kupata mashine ndogo ndogo zitakazorahisisha uchakataji wa mbolea na viuatilifu ili vipatikane kwa wakati," amesema.
Mkurugenzi huyo amesema mradi hiyo mipya itahusisha wahusika walewale na kwamba lengo ni kuona maboresho zaidi.
Amesema moja ya mafanikio makubwa ya mradi uliopita ni kuunganisha wakulima na wauzaji, jambo linalopelekea miradi mipya kusonga mbele kutatua changamoto zilizobaki.
Amesema pia katika kipindi cha awali, wamefikia shule 15 ambapo shule 11 Arusha DC na shule nne Karatu ambazo zimeanzishiwa mashamba ya kilimo ikolojia ili watoto wapate mboga na matunda.
Ayesiga amesema miradi mipya inaenda kufikia wanafunzi wote ikiwemo wale wenye changamoto ya lishe na uwezo wa wazazi wengine kuchangia chakula mashuleni kuwa mdogo.
"Kuna wazazi hawawezi kuchangia chakula si kwa kutokupenda, bali kwa hali ngumu ya kimaisha. Hivyo awamu hii ya pili itaangalia namna ya kuziba mwanya huo ili watoto wote wapate chakula kwa usawa," amesema.








No comments:
Post a Comment