Mc DONALD YAGAWA MBOLEA KWA WAKULIMA WA PEMBA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Friday, September 25, 2026

Mc DONALD YAGAWA MBOLEA KWA WAKULIMA WA PEMBA


NA MWANDISHI WETU

KAMPUNI ya McDonald Organic Horticulture and Soil Specialist Ltd imegawa mbolea hai aina ya Volca Grow kwa wakulima kutoka Pemba wanaoshiriki Tamasha la Kilimo Hai Zanzibar (ZOF) linaloendelea Dole Kizimkazi, Unguja Zanzibar.


Mbolea hizo zimegawiwa leo na Ofisa Uchechemuzi wa Mwamvuli wa Kilimo Hai Tanzania (TOAM), Paul Chilewa kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Donald Mwakamele.


Akizungumza wakati wa ugawaji huo, Chilewa alisema Volca Grow ni mbolea inayotengenezwa kwa kutumia mwamba wa asili (volcanic rock) na inasaidia kurejesha rutuba ya udongo na kuamsha viumbe hai (microbiology) muhimu kwa ukuaji wa mimea.


"Udongo wetu mwingi umeharibika kutokana na matumizi ya muda mrefu ya mbolea na viuatilifu vya kemikali, hasa huku Zanzibar. Tumeleta mbolea hii kwa majaribio, na imefanya vizuri sana maeneo mengi kama Mbeya kwenye kahawa na korosho," alisema.


Aliongeza kuwa mbolea hiyo imeleta mwamko mkubwa kwa wakulima wa Zanzibar licha ya kuleta kiasi kidogo cha maonesho.


"Tulikuja na chache za kuonyesha lakini uhitaji ni mkubwa. Mbolea hii ni tofauti, ukiweka mara moja hutahitaji kuweka tena kwa miaka mitatu hadi minne, na inafaa kwa mazao yote - mbogamboga, matunda, na mazao ya miti. Huharibu udongo na mazao hayabaki na mabaki ya kemikali yenye athari kwa afya ya binadamu," alifafanua.


Chilewa alisema kampuni inaendelea na taratibu za kisheria na serikali ya Zanzibar kuhakikisha mbolea hiyo inapatikana kwa wingi na kwa bei nafuu.


"Tuko kwenye mchakato wa kukamilisha utaratibu wa kuingiza bidhaa Zanzibar. Tulileta sampuli. Sasa tunaongea na serikali na mamlaka husika ili ipate jina rasmi huku na iweze kuingia kwa wingi," alisema.


Alibainisha kuwa Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi, pia amepewa sampuli ya mbolea hiyo.


Amesema wakulima wa Pemba wamepewa kipaumbele kwa sababu ya umbali na gharama za usafiri, lakini pia wakulima wachache wa Unguja wameshapatiwa awali. Kampuni inapanga kuanzisha mashamba darasa ili wakulima wajifunze matumizi sahihi.


Wakulima washukuru


Baadhi ya wakulima walioipata mbolea hiyo wameishukuru kampuni na kuahidi kuifanyia kazi na kutoa mrejesho wa matokeo.


"Jina langu naitwa Mwashamba Ameir Juma*, nimetokea ushirika wa kilimo Kizimbani. Tunajishughulisha na mazao yote - mbogamboga na miti mikubwa. Tunashukuru tumepata mbolea ya kwenda kuijaribu kuona kama kweli ukiweka mara moja hudumu kwa miaka mitatu bila kuweka tena na mavuno yakoje," alisema.


Naye mkulima wa kilimo hai, Salama Hussein Makame, alisema "Mimi ni mkulima wa karafuu, parachichi, duriani na mbogamboga aina zote. Tunashukuru kwa viongozi kutupatia mbolea hii. Sio majaribio tu, ni kazi ya kuitumia na kuona matokeo. Naamini matokeo yatakuwa sahihi kwa asilimia 100. Tutakuwa nao bega kwa bega katika harakati zetu za kilimo."


Ugawaji huo ni sehemu ya juhudi za kukuza matumizi ya pembejeo hai na kupunguza matumizi ya kemikali hatarishi katika kilimo visiwani Zanzibar.

No comments:

Post a Comment