NA MWANDISHI WETU, IRINGA
WANANCHI wa Mkoa wa Rukwa wanatarajiwa kuanza kunufaika na huduma ya umeme wa uhakika pale Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa Kilovoti 400 wa Iringa–Kisada–Mbeya–Tunduma–Sumbawanga (TAZA) utakapokamilika hatua itakayochochea maendeleo ya kiuchumi, uwekezaji na utoaji wa huduma bora za kijamii katika mkoa huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, amesema kukamilika kwa mradi huo kutaiwezesha Rukwa kuunganishwa kwenye Gridi ya umemem ya Taifa kwa mara ya kwanza, jambo litakaloongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi, taasisi za umma, viwanda na wafanyabiashara.
Akizungumza Oktoba 24, 2026 wakati wa kikao na wakandarasi wa mradi huo, Twange amewataka wakandarasi wa mradi huo kuhakikisha unakamilika ifikapo Novemba 15, 2026 ili wananchi waanze kupata manufaa yaliyokusudiwa.
“Huu ni mradi mkubwa wa kimkakati wenye urefu wa kilomita 616 na gharama ya takribani Shilingi trilioni 2. Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huu mkubwa katika sekta ya nishati. Kukamilika kwa mradi huu kutawapatia wananchi wa Rukwa umeme wa uhakika na kufungua fursa mpya za maendeleo ya kiuchumi,” amesema Bw. Twange.
Amesema kuwa mpaka sasa mradi huo umefikia asilimia 96.57 ya utekelezaji wake na utakapokamilika utaongeza uwezo wa Gridi ya Taifa kusafirisha umeme, kupunguza changamoto za upatikanaji wa umeme katika maeneo ya Kusini Magharibi mwa Tanzania na kuweka mazingira bora ya uwekezaji katika sekta za viwanda, madini, biashara na kilimo.
Kwa wananchi wa Rukwa, mradi huo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma bora katika hospitali, shule na taasisi nyingine za kijamii zinazotegemea umeme, huku ukiimarisha shughuli za uzalishaji mali na ajira kupitia uwekezaji unaotegemea nishati ya uhakika.
Aidha, Twange amesema mradi huo una umuhimu wa kikanda kwani utakamilisha maandalizi ya kuunganisha mifumo ya umeme ya Tanzania na Zambia, hatua itakayowezesha biashara ya umeme kati ya nchi hizo mbili na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Akizungumzia baadhi ya changamoto zilizochelewesha mradi huo ni pamoja na usafirishaji wa vifaa vikubwa, hususan transfoma zenye uzito wa zaidi ya tani 200, ambazo zilihitaji maandalizi maalum ya miundombinu ya barabara kabla ya kusafirishwa.
Hata hivyo, TANESCO inaendelea kushirikiana kwa karibu na TANROADS kuhakikisha vifaa vilivyosalia vinafikishwa salama katika maeneo ya mradi ili kazi zote zikamilike ndani ya muda uliokubaliwa.
Mradi wa TAZA, ambao awali ulitarajiwa kukamilika Mei 2026, sasa unatarajiwa kukamilika Novemba 15, 2026, ukiwa sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa Watanzania na kuharakisha maendeleo ya uchumi wa taifa.










No comments:
Post a Comment