![]() |
NA MWANDISHI WETU
MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Organic Moringa Herbal Products, Dk Sebastian Msapalla amesema ushiriki wake katika Tamasha la Kilimo Hai Zanzibar (ZOF), umempa fursa ya kujitangaza na kuuza bidhaa asilia zinazotokana na kilimo hicho, huku akisisitiza elimu zaidi.
Akizungumza katika Banda la Shirika la Island of Peace (IDP), ambalo limewezesha kushiriki maonesho hayo yanayofanyika katika Viwanja vya Dole Kizimbani Unguja Zanzibar, amepongeza taasisi ya Parmacultural Paractical Institute Zanzibar (PPIZ), kwa kuandaa tamasha hilo muhimu kwa wadau wa kilimo hai.
"Tumekuja hapa na wageni mbalimbali, wakiwemo viongozi, na tumefurahi kupata watu waliokuja kutazama bidhaa zetu. Tumejitangaza na tumefanikiwa kuuza, ila tuongeze kasi ya kutoa elimu ya kilimo hai," amesema.
Hata hivyo, Dk Msapalla alibainisha changamoto mbili zinazokwamisha mafanikio makubwa ya tamasha hilo kuwa ni kukosa matangazo na umbali.
Amesema eneo la tamasha liko mbali kidogo kutoka mjini, na matangazo hayakufanyika kwa muda mrefu, hali iliyowafanya watu wengi kushindwa kufika.
"Kuna kaumbali kidogo kutoka mjini, si kila mtu anaweza kufika kirahisi. Pamoja na hayo, matangazo yamekuwa mafupi. Kama wangepewa muda mrefu zaidi, watu wangeweza kufika kwa wingi kutembelea na kununua bidhaa," alieleza.
Pili ni uelewa mdogo wa dhana ya kilimo hai kwamba licha ya hamasa, bado dhana ya kilimo hai na bidhaa asilia ni ngeni kwa watu wengi, sio Zanzibar tu bali Tanzania nzima.
"Kwa vile tunahamasisha kilimo hai, jambo hili limeonekana kama geni ambalo halijazoeleka sana. Bado ni jambo ambalo tunatakiwa kupiga mbiu kwa wingi ili watu wafahamu faida zake. Ni kama mapinduzi ya kijani kwa afya ya binadamu," amesema.
Amesema licha ya changamoto hizo, mambo yamekwenda vizuri na amewashukuru waandaaji na IDP likiongozwa na Richard Libent kwa kufanikisha ushiriki wao. "Tumejitangaza, tumeuza, na tumepata uzoefu. Tunawashukuru sana IDP," alihitimisha.





No comments:
Post a Comment