RAIS SAMIA ATAKA MIKOA, HALMASHAURI KUIMARISHA UKUSANYAJI WA MAPATO - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Wednesday, September 2, 2026

RAIS SAMIA ATAKA MIKOA, HALMASHAURI KUIMARISHA UKUSANYAJI WA MAPATO


NA OWM - TAMISEMI, ZANZIBAR


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Viongozi wa Mikoa na Wilaya kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kudhibiti matumizi na kuelekeza rasilimali katika vipaumbele vya maendeleo, hususan sekta za elimu na afya.


Rais Dkt. Samia ametoa maagizo hayo leo Septemba 2, 2026, wakati wa hafla ya kuwaapisha Wakuu wa Mikoa na Katibu Tawala wa Mkoa iliyofanyika Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar.


“Kila mwenye eneo lake la utawala ajitahidi kuhakikisha mambo yanaenda katika eneo lake; si kila kitu kitoke kwenye Hazina ya Serikali,” amesema Rais Dkt. Samia.


Aidha, amezitaka Halmashauri kuziba mianya ya upotevu wa mapato na kuimarisha utoaji na urejeshaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, huku mikopo hiyo ikielekezwa katika miradi inayozalisha.


Pia, ameelekeza mapato ya ndani yatumike kupanua na kujenga masoko, kuweka mazingira bora kwa wafanyabiashara wadogo na kugharamia miradi ya maendeleo. Amesisitiza kuwa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025 na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji viongozi kuwajibika na kusimamia matokeo.


Walioapishwa kuwa Wakuu wa Mikoa ni Mhe. Jumanne Abdallah Sagini wa Mbeya, Mhe. Alexander Pastory Mnyeti wa Geita, Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo wa Pwani na Mhe. CP Salum Rashid Hamduni wa Mwanza. Bw. Richard Marcellino Kayombo ameapishwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani.




No comments:

Post a Comment