BRELA NA COSTECH ZAZINDUA PROGRAMU YA InnoIP KUIMARISHA ULINZI WA MILIKI UBUNIFU NCHINI - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Saturday, August 22, 2026

BRELA NA COSTECH ZAZINDUA PROGRAMU YA InnoIP KUIMARISHA ULINZI WA MILIKI UBUNIFU NCHINI



NA MWANDISHI WETU 

WAKALAwa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia Dar Teknohama Business Incubator (DTBi) na Buni Innovation Hub, leo tarehe 22, 2026 imezindua Programu ya InnoIP ambayo imelenga kuimarisha mfumo wa ubunifu nchini Tanzania.


Programu hiyo imezinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Salha Burian katika hafla iliyohudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dkt. Amos Nungu na Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu kutoka BRELA, Bi. Loy Mhando ambaye alimwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Salha Burian alitoa wito kwa wawekezaji, taasisi za kifedha, kampuni na sekta binafsi kushirikiana na wabunifu wa Kitanzania ili kuendeleza na kuleta thamani ya ubunifu nchini.


“Ulinzi wa miliki ubunifu unakuwa na maana kiuchumi pale miliki hiyo inapotumiwa kwa uwajibikaji katika kuanzisha biashara, kuboresha huduma, kuvutia uwekezaji, kuzalisha ajira na kujenga thamani,” alisema Mhe. Balozi Dkt. Burian.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu kutoka BRELA, Loy Mhando, alisema lengo kuu la Programu ya Ubunifu na Miliki Ubunifu (InnoIP) ni kuimarisha mfumo wa ubunifu nchini Tanzania kwa kuwawezesha wabunifu, kampuni changa, watafiti na wafanyabiashara kutambua, kulinda, kusimamia kibiashara haki za miliki ubunifu ili kuleta thamani ya kiuchumi na kijamii.


“Programu hii itahudumia kampuni changa, wabunifu walio katika hatua za awali, watafiti, wanafunzi wa vyuo vikuu, biashara ndogo na za kati, biashara zinazoongozwa na wanawake na vijana, wajasiriamali katika sekta za ubunifu, vituo vya ubunifu, vituo vya uatamiaji wa biashara pamoja na taasisi za utafiti” Alisema Bi. Mhando.


Naye, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, alibainisha kuwa programu hiyo inalenga kubadili namna ubunifu unavyotazamwa nchini Tanzania, akisisitiza kuwa miliki ubunifu si suala la kisheria pekee, bali ni rasilimali muhimu ya kiuchumi.


“Hataza, Hakimiliki na aina nyingine za miliki ubunifu zinaweza kuwa msingi wa kuvutia uwekezaji, kutoa leseni, kuhawilisha teknolojia na kujenga biashara zinazoweza kukua,” alisema Dkt. Nungu.


Dkt. Nungu aliongeza kusema kuwa katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa programu hiyo, lengo ni kuwafikia watu wasiopungua 5,000, kufanya tathmini ya mahitaji ya miliki ubunifu kwa wabunifu wasiopungua 120, pamoja na kusaidia hatua muhimu za ulinzi wa miliki ubunifu zisizopungua 20.


Programu ya InnoIP imezinduliwa ikiwa na Kauli Mbiu isemayo: “Kutoka Wazo hadi Fursa za Miliki Bunifu: Kulinda Ubunifu Kujenga Thamani na Kuharakisha Ubiasharishaji


Kupitia programu hiyo, wadau wanatarajiwa kuona ongezeko la ubunifu uliolindwa, biashara zilizoendelezwa, uwekezaji na ajira zilizozalishwa, hatua inayolenga kuchochea ukuaji wa uchumi unaotegemea maarifa, teknolojia na ubunifu nchini Tanzania.





No comments:

Post a Comment