PROF. SHEMDOE AWAASA VIONGOZI SERIKALI ZA MITAA KUEPUKA MIGOGORO ILI KUONGEZA UFANISI WA HUDUMA KWA WANANCHI - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Friday, August 21, 2026

PROF. SHEMDOE AWAASA VIONGOZI SERIKALI ZA MITAA KUEPUKA MIGOGORO ILI KUONGEZA UFANISI WA HUDUMA KWA WANANCHI


NA OWM TAMISEMI, DODOMA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, amewaasa viongozi katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuepuka migogoro miongoni mwao na baina yao na watumishi wanaowaongoza, akisisitiza kuwa migogoro mahali pa kazi inakwamisha ufanisi na azma ya Serikali ya kuwapelekea wananchi huduma bora.


Prof. Shemdoe ametoa wito huo leo, Agosti 21, 2026, wakati akifunga Mkutano Mkuu wa 16 wa Mwaka wa Taasisi ya Maboresho katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (TOA), uliofanyika kwa siku tatu kuanzia Agosti 19 hadi 21, 2026, katika Ukumbi wa Jiji  Mtumba, jijini Dodoma.


“Niwaase na kuwaomba sana muepuke migogoro miongoni mwenu; kati ya Mkurugenzi na Katibu Tawala, kati ya Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya, kati ya RAS na Mkuu  wa Mkoa, na kati ya kiongozi na watumishi unaowaongoza. Mahali penye migogoro hakuna ufanisi wa kazi na maendeleo,” amesema Prof. Shemdoe.


Amesema viongozi na watumishi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wanapaswa kufanya kazi kwa kuheshimiana, akisisitiza kuwa hakuna sababu kwa Mkurugenzi wa Halmashauri kupambana na Mwenyekiti wa Halmashauri au Mstahiki Meya.


Prof. Shemdoe amesema uzoefu wake katika uongozi umemfundisha umuhimu wa ushirikiano na kuheshimiana, akieleza kuwa alipokuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hakuwahi kugombana na Mwenyekiti wa Halmashauri, na alipokuwa Katibu Tawala wa Mkoa hakuwahi kupishana lugha na Mkuu wa Mkoa.


Aidha, Prof. Shemdoe amewataka viongozi hao kutumia maarifa, weledi na uzoefu wao katika kuwatumikia wananchi, akieleza kuwa Serikali za Mitaa ziko karibu zaidi na wananchi na hivyo ni kimbilio lao katika kupata huduma mbalimbali.

Amesema wananchi wanapopima mafanikio ya Serikali, kwa kiasi kikubwa huyapima kupitia huduma wanazozipata katika maeneo yao, zikiwemo huduma za afya ya msingi, elimu ya msingi, usafiri na usafirishaji.


Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe ametumia fursa hiyo kumshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuidhinisha na kuleta fedha kwa ajili ya uendeshaji wa Taasisi za Umma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.


Amesema fedha hizo zinaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kufanya shughuli za kiuchumi na kujiingizia kipato kwa ajili ya kuendesha maisha yao.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Maboresho katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (TOA), Albert Gabriel Msovela, amemhakikishia Prof. Shemdoe kuwa wajumbe wa taasisi hiyo ni askari wake kiutendaji na kwamba TOA itaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi kwa mujibu wa Katiba.


Msovela amesema TOA itaendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza malengo mbalimbali ya kitaifa, ikiwemo utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


“Mhe. Waziri, naomba nikuhakikishie kwamba kupitia Mkutano Mkuu huu wa 16 wa Mwaka wa TOA, tutatoka na mikakati, maazimio pamoja na mipango madhubuti ambayo tutakwenda kuwashirikisha wananchi katika utekelezaji wake kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo,” amesisitiza Bw. Msovela.


Mkutano Mkuu wa 16 wa Mwaka wa TOA uliowakutanisha Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Makatibu Tawala wa Wilaya, umefanyika chini ya Kaulimbiu isemayo: “Ugatuzi wa Madaraka katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ni Nguzo Madhubuti ya Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”





No comments:

Post a Comment