NA MWANDISHI WETU, UGANDA
Serikali za Tanzania na Uganda zimekutana kujadili utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya mafuta na gesi kati ya nchi hizo mbili.
Hayo yamebainishwa tarehe 17 Septemba 2026 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia masuala ya Mafuta na Gesi Asilia Tanzania, Dkt. James Mataragio, wakati wa kikao cha pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Maendeleo ya Madini nchini Uganda, Ireni Paulene Bateebe, kilichofanyika Mjini Kampala, Uganda.
Dkt. Mataragio amesema kuwa katika kikao hicho, viongozi hao wamejadili namna ya kutekeleza miradi mbalimbali ya nishati, ikiwemo Bomba la Kusafirisha Bidhaa za Mafuta Safi, Marine Storage Terminal katika Bandari ya Tanga, pamoja na mpango wa kusafirisha gesi asilia kutoka Tanzania kwenda Uganda.
Amesisitiza kuwa matokeo ya kikao hicho ni sehemu ya juhudi za Serikali za Tanzania na Uganda katika kuimarisha ushirikiano katika sekta ya nishati na kuhakikisha miradi ya pamoja inatekelezwa kwa ufanisi, wakati ambapo Tanga inaendelea kujengwa ili kuwa kitovu mahususi cha masuala ya nishati kwa ajili ya kuhudumia Tanzania na nchi nyingine za ukanda huo.
Katika hatua nyingine, wakiwa nchini humo, viongozi hao walipata wasaa wa kushiriki uzinduzi wa Matanki ya Kuhifadhia Mafuta nchini humo (Kampala Storage Terminal).
Katika kikao hicho Dkt. Mataragio aliambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mussa Makame, pamoja na Kamishna wa Petroli Wizara ya Nishati, Godluck Shirima.








No comments:
Post a Comment