TANZANIA imejitokeza katika uongozi wa ushirikiano wa sayansi barani Afrika kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), ambayo inaongoza eneo la kuimarisha uwezo wa taasisi za ufadhili wa tafiti katika awamu ya tatu ya SGCI.
Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk Amos Nungu, aliwasilisha mwelekeo wa eneo hilo jana Jumanne katika Mkutano wa Washirika Wote wa SGCI mjini Windhoek. Alisema uwezo wa taasisi za Afrika kupanga, kufadhili na kusimamia tafiti ndio msingi wa ushirikiano wenye matokeo.
“Nguvu ya muungano hupimwa kwa yale ambayo wanachama wake wanaweza kuyafanya kwa uthabiti na kwa pamoja,” alisema.
Nafasi hiyo inaiweka Tanzania katika mjadala wa namna nchi za Afrika zitakavyojenga taasisi zenye uwezo wa kusimamia uwekezaji wa pamoja katika sayansi. COSTECH pia ni sehemu ya kundi la uratibu wa mabaraza ya SGCI, pamoja na taasisi kutoka Ghana, Afrika Kusini, Kenya na Namibia. Ghana ndiyo inayoongoza muungano huo.
Dk Nungu alisema changamoto za afya, usalama wa chakula, mabadiliko ya tabianchi na teknolojia haziishii kwenye mipaka ya taifa moja. Kutokana na hali hiyo, taasisi za ufadhili zinahitaji uwezo wa kufanya kazi na wenzao, kuoanisha taratibu pale inapofaa na kusimamia miradi inayohusisha nchi kadhaa.
Alisema fedha za utafiti zitakuwa na thamani kubwa zaidi ikiwa taasisi zitachagua vipaumbele kwa umakini, zitatathmini maombi kwa uadilifu, zitafuatilia miradi na kuhakikisha matokeo yake yanawafikia watunga sera na wananchi.
Katika jopo hilo, Dk Cephas Adjei Mensah wa Ghana alieleza muundo wa SGCI na namna taasisi za Afrika zinavyoshirikiana na wafadhili na washirika wa kitaalamu. Dk Angus Paterson wa Afrika Kusini alizungumzia fursa za kuendeleza ushirikiano huo, huku Prof Dickson Andala wa Kenya akielekeza mjadala kwenye ufadhili wa tafiti za pamoja na matumizi ya matokeo yake. Jopo liliongozwa na Prof Anicia Peters wa Namibia na kufuatiliwa na wawakilishi wa taasisi zinazoshiriki SGCI.
Uongozi wa Tanzania katika eneo la kujenga uwezo unakuja wakati SGCI imeanza awamu ya miaka mitano, kuanzia 2026 hadi 2030. Awamu hiyo ina ahadi ya dola za Canada milioni 57, sawa na takribani dola za Marekani milioni 42, kwa shughuli za mpango katika nchi zinazoshiriki. Mgao maalumu wa Tanzania haujatangazwa.
Nafasi ya COSTECH pia inaendana na mwelekeo wa sera ya mambo ya nje ya Tanzania, inayosisitiza ushirikiano wa Afrika, diplomasia ya uchumi na ushiriki katika taasisi za kikanda na kimataifa. Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kuimarisha tafiti na kuipa Tanzania nafasi ya kuwa kitovu cha ubunifu katika ukanda huu.
Dk Nungu alisema kipimo cha mafanikio hakitakuwa idadi ya mikutano, bali uwezo wa taasisi kuendesha programu bora, kuwafikia watafiti wengi zaidi, kushirikiana kuvuka mipaka na kuonesha namna tafiti zinavyosaidia maamuzi na maisha ya watu.






No comments:
Post a Comment