NA MWANDISHI WETU
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza uwepo wa mvua za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mbalimbali nchini kuanzia Novemba mwaka huu hadi Aprili 2027, huku wananchi wakitakiwa kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 23,2026 baada ya semina maalumu iliyofanyika Oktoba 22, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa TMA,Dkt.Ladislaus Chang'a amesema mvua za juu ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Dodoma, Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe, Rukwa na maeneo ya kusini mwa Morogoro.
Amesema mwelekeo huo wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka utaathiriwa kwa kiasi kikubwa na hali ya El Niño yenye nguvu kubwa, hususan katika kipindi cha Novemba 2026 hadi Januari 2027.
Ametaja mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi inatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Kwa mujibu wa Dkt.Chang'a amesema mvua hizo zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya Oktoba katika baadhi ya maeneo ya Tabora, Katavi, Kigoma, Lindi na Mtwara, kabla ya kusambaa katika maeneo mengine mwezi Novemba mwaka huu na kuisha kati ya wiki ya tatu na ya nne ya Aprili 2027.
Ameeleza kuwa hali hiyo inachangiwa na ongezeko la joto la bahari katika eneo la tropiki ya kati ya Bahari ya Pasifiki, linaloashiria kuendelea kwa El Niño yenye nguvu kubwa, pamoja na joto la bahari upande wa magharibi wa Bahari ya Hindi na upepo wenye unyevunyevu kutoka misitu ya Kongo.
Amesema mifumo hiyo ya hali ya hewa inatarajiwa kuimarisha upatikanaji wa mvua katika maeneo mengi nchini, hali inayohitaji maandalizi ya mapema ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza
Katika sekta ya kilimo, TMA imewashauri wakulima kuandaa mashamba mapema, kuchimba mifereji na kutengeneza matuta ya kuzuia maji kutuama, pamoja na kutumia mbegu zinazofaa kwa mazingira ya maeneo yao.
Kwa upande wa mifugo na uvuvi, mamlaka hiyo imeeleza kuwa ongezeko la mvua linaweza kuongeza upatikanaji wa malisho, lakini wafugaji wanapaswa kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya milipuko, yakiwamo homa ya bonde la ufa.
Aidha, taasisi zinazohusika na usafirishaji na ujenzi zimetakiwa kukagua miundombinu mara kwa mara ili kupunguza uharibifu unaoweza kusababishwa na mvua nyingi katika barabara, madaraja na reli za MGR na SGR.
TMA pia imeeleza kuwa ongezeko la maji katika mabwawa linaweza kusaidia uzalishaji wa umeme, huku mamlaka zinazohusika na afya na maji zikitakiwa kulinda vyanzo vya maji na kuimarisha hatua za kuzuia magonjwa ya milipuko.
Katika hatua nyingine, menejimenti za maafa na mamlaka za serikali za mitaa zimetakiwa kuimarisha kamati za maafa kuanzia ngazi ya vijiji ili kuhakikisha tahadhari za mapema zinatolewa na wananchi wanapata taarifa kwa wakati.
Amewataka wananchi wananchi kuendelea kufuatilia utabiri wa hali ya hewa wa saa 24, siku 10 na mwezi unaotolewa na mamlaka hiyo kwa ajili ya kupanga shughuli zao na kuchukua tahadhari zinazofaa.
Vilevile, vyombo vya habari vimetakiwa kusambaza taarifa rasmi za hali ya hewa zinazotolewa na TMA pekee.
TMA imekumbusha kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019, ni kosa kisheria kusambaza taarifa za hali ya hewa kutoka vyanzo visivyo rasmi.







No comments:
Post a Comment