NA MAGENDELA HAMISI
MFUKO wa Taifa wa Huduma Ndogo za Kifedha Self Microfinance Fund katika kipindi cha miaka mitatu imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya takribani Sh mil. 138 na kuingiza faida ya bil. 3.19.
Imeelezwa kwamba hatua hiyo imesaidia kuwawezesha wananchi kiuchumi na kuchangia upatikanaji wa ajira 262, 624 na mikopo ikilenga kusaidia wananchi kuanzisha na kukuza shughuli za kiuchumi, wakiwemo wakulima, wavuvi, vijana, wafanyabiashara na watumishi wa umma, ili kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.
Hayo yamebainishwa leo jijinj Dar es Salaam na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Santiel Yona katika kikao kazi kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Aidha amebainisha kwamba mikopo yanayoitoa imegawanyika katika makundi mbalimbali, ikiwemo mikopo inayotolewa kwa taasisi na vyama vya kifedha ili viweze kuwakopesha wananchi, pamoja na mikopo inayotolewa moja kwa moja kwa walengwa.
Alisema pamoja na kutoa mikopo, taasisi hiyo imekuwa ikitoa elimu ya fedha kwa wateja wake ili kuwasaidia kuelewa masharti ya mikopo, viwango vya riba, namna ya kurejesha fedha na jinsi ya kutumia mikopo katika shughuli zinazoweza kuleta faida. Alisisitiza kuwa elimu hiyo ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanakopa kwa kuzingatia uwezo wao wa kurejesha fedha.
"Pia tunatoa huduma mbalimbali za kifedha, zikiwemo bima zinazolenga kuwasaidia wateja kukabiliana na majanga yanayoweza kuathiri shughuli zao za kiuchumi na pi tumekuwa tukibuni bidhaa za mikopo zinazolenga makundi maalumu, ikiwemo vijana wanaotaka kujiajiri kupitia shughuli kama usafiri wa bajaji na wananchi wanaohitaji mikopo ya nishati safi.
Ameongez kuwa Katika kipindi hicho Cha miaka mitatu kuanzia 2023 hadi 2026 wamefanikiwa kupata faida ya Sh bilioni 3.19 na kutoa gawio la Sh milioni 490 kwa Serikali. Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, mafanikio hayo yanaonesha uwezo wa taasisi kuendelea kujiendesha, kukuza mtaji wake na kurejesha sehemu ya mapato kwa Serikali kama taasisi ya umma.
Pia amesema kwamba, SELF Microfinance ina mtandao wa matawi 12 pamoja na vituo viwili vya huduma katika baadhi ya maeneo nchini.
Aidha ameeleza kuwa taasisi hiyo inalenga kupanua wigo wa kuwafikia wananchi katika mikoa mbalimbali kwa kuimarisha huduma za kidijitali, ili wateja waweze kupata huduma za kifedha kwa urahisi bila kutegemea uwepo wa tawi katika maeneo yao.
Akizungumzia changamoto zinazokabili sekta ya mikopo kuwa ni pamoja na uelewa mdogo wa elimu ya fedha, baadhi ya wakopaji kutokuwa na utamaduni wa kurejesha mikopo kwa wakati na changamoto zinazohusiana na biashara zisizo rasmi. Imeeleza kuwa itaendelea kutoa elimu kwa wateja na kufuatilia matumizi ya mikopo ili kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Aidha amesisitiza kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali, taasisi nyingine na wadau mbalimbali katika kuimarisha huduma za kifedha na kuwawezesha wananchi kiuchumi, hususan vijana na makundi yanayohitaji mitaji ya kuanzisha au kupanua shughuli za uzalishaji. Hatua hiyo inalenga kuongeza ajira, kukuza kipato cha wananchi na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.





No comments:
Post a Comment