NA MWANDISHI WETU
UWEZO wa uzalishaji wa umeme nchini umeongezeka hadi kufikia megawati 6,496 kutokana na kukamilika kwa baadhi ya miradi ya nishati, huku Serikali ikiendelea na mikakati ya kuongeza uzalishaji hadi kufikia megawati 8,000 ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wananchi na viwanda.
Waziri wa Nishati, Juma Homera, amesema hayo leo Octoba 18,2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya sekta ya nishati, akibainisha kuwa uwekezaji unaofanywa na Serikali unalenga kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini.
Amesema umeme unaozalishwa unatokana na vyanzo mbalimbali, ikiwamo maji, gesi asilia na jua, huku mradi wa nishati ya jua wa Kishapu ukiwa tayari umeanza kufanya kazi kwa uwezo wa zaidi ya megawati 50 na Serikali ikiingia mkataba mwingine wa kuzalisha megawati 100 katika eneo hilo.
Homera amesema Serikali pia inaendelea kuwekeza katika nishati jadidifu, ambapo miradi ya kuzalisha megawati 600 kwa kutumia nishati hiyo ipo katika hatua mbalimbali za majadiliano na upembuzi yakinifu, hatua inayotarajiwa kuongeza uwezo wa uzalishaji na kupunguza hatari ya upungufu wa umeme.
Amesema sambamba na kuongeza uzalishaji, Serikali inaimarisha miundombinu ya kusafirisha umeme ili kuhakikisha unawafikia watumiaji kwa uhakika, akieleza kuwa njia ya kusafirisha umeme ya Chalinze hadi Dodoma imekamilika tangu Septemba mwaka huu na imeimarisha usambazaji wa umeme katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Ameongeza kuwa mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Iringa kupitia Tunduma hadi Sumbawanga unatarajiwa kuanza kutumika Novemba mwaka huu, huku ukitarajiwa kuimarisha upatikanaji wa umeme katika Nyanda za Juu Kusini na kuweka fursa ya kuuza umeme nchini Zambia.
Aidha Homera amesema kuwa, mradi mwingine wa Chalinze–Kinyerezi–Mkuranga unatarajiwa kuanza kutumika Februari mwakani, ukiwa na lengo la kuboresha upatikanaji wa umeme jijini Dar es Salaam na maeneo ya viwanda vya Mkuranga ili kuchochea uwekezaji na uzalishaji wa bidhaa.
Amesema ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Songea kupitia Tunduru na Masasi hadi maeneo ya Lindi na Mtwara unaendelea, ukiwa na lengo la kuyaunganisha maeneo hayo na gridi ya taifa na kupunguza changamoto za upatikanaji wa umeme.
Homera amesema mahitaji ya umeme nchini yanaendelea kuongezeka kutokana na kuongezeka kwa viwanda na wawekezaji, hukubakibainisha kuwa matumizi ya umeme nyakati za usiku yamefikia zaidi ya megawati 2,004 kwa wakati mmoja, jambo linaloonesha umuhimu wa kuendelea kuongeza uzalishaji na uwezo wa usafirishaji.
Amesema Serikali pia inaendelea kufanya tafiti kuhusu vyanzo vingine vya nishati, ikiwamo jotoardhi na maji, ili kuongeza chaguo la uzalishaji wa umeme na kuhakikisha nchi ina uwezo wa kukidhi mahitaji ya sasa na yajayo.
Akizungumzia sekta ya gesi na mafuta, amesema Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linaendelea na shughuli za utafutaji katika maeneo mbalimbali, yakiwamo Lindi, Mtwara, Songosongo Magharibi na Mnazi Bay, huku ukusanyaji wa taarifa za mitetemo ukiendelea katika vitalu vya utafutaji.
Amesema maandalizi ya uchimbaji wa kisima cha uzalishaji na uwekaji wa mitambo ya kusafirisha gesi katika kitalu cha Ntorya yanaendelea, huku uzalishaji wa gesi ukitarajiwa kufikia futi za ujazo milioni 40 kwa siku, hatua itakayosaidia upatikanaji wa nishati kwa matumizi ya viwanda na uzalishaji wa mbolea.





No comments:
Post a Comment