NA MWANDISHI WETU
MENEJA wa Wakala wa Mafunzo ya Mifugo (LITA), Kituo cha Mabuki Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, Jacob Ngowi amesema elimu ya vitendo kwa wanafunzi wa Astashahada na Stashahada katika chuo chao, yamesaidia kuleta mabadiliko kwa wafugaji.
Ngowi ameyasema hayo hivi karibubni wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii chuoni hapo ambapo amelishukura Shirika la Kilimo Endelevu (SAT), kwa kuja na Mradi wa Kusaidia Utekelezaji wa Mitaala kwa Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo (CISTI).
Meneja huyo alisema kwa muda mrefu katika vyuo hivyo, wakufunzi wamekuwa wakifundishwa sayansi ya ujuzi katika eneo la mifugo, ila ujio wa mradi huo, umeleta mabadiliko makubwa kwa wanafunzi wao.
“Sisi wakufunzi tunawafunzi zile sayansi za kuwapatia ujuzi namna ya kwenda kufanya wanapoenda kwenye vituo vya kazi, ila ujio wa mradi huo unatekelezwa na Shirika la Kilimo Endelevu Tanzania umeleta ujuzi na maarifa zaidi,” alisema.
Meneja huyo alisema wanafunzi wamepokea mafunzo hayo ya vitendo vizuri, jambo ambali linarahisisha utekelezaji.
Alisema wanafunzi watakuwa mabalozi wazuri kwa jamii ya wafugaji, ambao wengi wamekuwa wakitumia mbinu za kizamani katika ufugaji.
Waziri wa Elimu wa Serikali ya Wanafunzo Chuo cha Mabuki, Frank Kubija alisema mafunzo ambayo wanapata yamewafungua kwa asilia kubwa, hali ambayo inawajengea kujiamini.
“Kusema kweli mafunzo haya yamekuwa na faida kubwa kwetu sisi kama wanafunzi wa chuo hiki, naamini tunaenda kutafsiri kwa vitendo haya ambayo tumejifunza, ili kuleta mageuzi katika sekta ya mifugo na uvuvi,” alisema.
Mwanafunzi huyo aliziomba taasisi na wadau wengine kuunga mkono juhudi ambazo zinafanywa na Shirika la Kilimo Endelevu, ili kuhakikisha sekta ya mifugo inaleta mageuzi chanya nchini.
Meneja Mradi huo, Kashindye Salum alisema wamekuwa wakitoa elimu ambayo inawawezesha wanafunzi kuhamisha maarifa wanayopata kwenda kwa wafugaji.
Kashindye alisema walikuja na mradi huo ili kuhakikisha vyuo vinazalisha wataalam wengi katika sekta ya mifugo na kilimo na matokeo mazuri yameanza kuonekana.
“Mradi huo umejikita katika kuwezesha wanafunzi kuhamisha maarifa yao na kwenda kuyatafsiri kivitendo kwa wafugaji na wakulima, ambao wanachangia pato la taifa,” alisema.
Meneja mradi huyo alisema wameweka mkazo katika kutoa mafunzo hasa kwa vyuo vya kilimo na mifugo, ili viweze kuzalisha wataalam wakutosha.
Kashindye alisema katika kipindi cha 2019–2025, mradi umefikia jumla ya watu 26,297 moja kwa moja. Walengwa hao ni pamoja na wakulima 6,647, wakiwemo wakulima mabingwa 174 wa kilimo hai; wakufunzi na watumishi wa menejimenti 1,530; wahudumu wa bustani 117; na wanafunzi 18,003.
Alisema kuanzia mwaka 2019 hadi Awamu ya Kwanza (2020–2022), mradi ulichangia katika uandaaji na upatikanaji wa machapisho manane ya marejeo ya kitaaluma, ambapo nakala 4,200 zilichapishwa na kusambazwa.
Alisema mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Liechtenstein (LED), una lengo la kusaidia taasisi za mafunzo ya kilimo za umma na binafsi kuzalisha wataalamu wenye umahiri wa kiufundi, wanaoweza kukidhi mahitaji ya soko la ajira, kueneza matumizi ya kilimo ikolojia na kuimarisha maisha ya wakulima wadogo na wafugaji.




No comments:
Post a Comment