SAMAKI AINA POTWE AIINGIZIA PWANI BIL. 9.5/- - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Sunday, November 1, 2026

SAMAKI AINA POTWE AIINGIZIA PWANI BIL. 9.5/-


NA MWANDISHI WETU 

MAPATO yatokanayo na utalii wa Samaki aina Papa Potwe Kisiwani Mafia mkoani Pwani, yamefikia Shilingi Bilioni 9.5 kwa mwaka 2025, huku idadi ya Papa Potwe ikipaa kutoka 100 mwaka 2012 hadi zaidi ya 268 mwaka 2025.


Hayo yamebainishwa na Baraka Kilopola, Kiongozi wa Mtandao wa Waongoza Watalii wa Papa Potwe Tanzania (WATON), taasisi inayojishughulisha na uhifadhi wa samaki hao  na elimu ya mazingira.


Amesema WATON wanajishughulisha na uhifadhi wa Papa Potwe na elimu kwa jamii ya Mafia wakiwemo wavuvi, wananchi wa kawaida na mashule.


Kilopola amesema wamejikita kumhifadhi Samaki Papa Potwe kwa sababu mbili kuu uchumi na sayansi.


"Kwanza, Papa Potwe anaingiza pato kubwa la utalii Kisiwani Mafia. Pili, ni mnyama aliye hatarini kutoweka kwa sababu uzalianaji wake ni mgumu. Tumeamua kumhifadhi ili vizazi vilivyopo na vijavyo viendelee kumuona na aendelee kukuza uchumi wa Mafia," amesema.


Alieleza kuwa Papa Potwe ndiyo samaki mkubwa kuliko wote duniani, lakini hana meno na haumi binadamu.


"Hili ndilo linalowavutia wageni unaweza kuogelea na samaki mkubwa hadi mita 8 bila kukudhuru. Madoa yake yanamvutia mtu kutaka kuogelea naye zaidi," amesema.


Kilopola amesema zamani wananchi walidhani Mafia kuna Papa Potwe 8 au 10 tu. Mwaka 2012, shirika la Marine Megafauna kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF) na Halmashauri ya Wilaya ya Mafia walifanya utafiti na kugundua Mafia kuna Papa Potwe 100 na zaidi. Baada ya kufanyia kazi changamoto, utafiti wa mwaka 2025 umethibitisha idadi imefikia 268 na inaendelea kukua.


Ongezeko hilo linatokana na mazingira salama, elimu kwa jamii, na ushirikiano kati ya WATON, WWF, Serikali na wavuvi.


Amesema kwa mujibu wa utafiti wa 2025, kila mgeni anayekuja Mafia kumuona Papa Potwe hutumia kati ya Dola za Marekani 1,000 hadi 1,500.


"Uchumi wa Mafia kwa ujumla kutokana na mnyororo wa thamani wa Papa Potwe ni Shilingi Bilioni 9.5. Halmashauri imekusanya mapato zaidi ya Shilingi Milioni 100 kutokana na tozo ya uhifadhi" amesema Kilopola.


Fedha hizo zinarudishwa kwa jamii kwa ajili ya maendeleo ya kijamii Mafia na zingine

zinazunguka kwenye mnyororo mzima - ajira hotelini, waongoza watalii, kampuni za ndege na pato la Taifa," amesema.


Kiongozi huyo Papa Potwe wanaonekana Mafia tu, kutokana na ukweli kuwa Mafia ni kisiwa kilichokaribiana na Mto Rufiji. "Mto Rufiji unazalisha chakula - uduvi - unaokuja Mafia. Eneo la Kilindoni limekaa kama herufi V, hivyo chakula kinakaa muda mrefu Kilindoni. Chakula kikiwa kingi, Papa Potwe wanakuwa wengi," alifafanua Kilopola.


Alitaja sababu ya pili ni uhifadhi endelevu ambapo Mafia ndiyo sehemu pekee Tanzania na Afrika unapoweza kumuona Papa Potwe kwa urahisi kwa sababu wanafanya utalii endelevu. 


"Maeneo mengine wanalisha wanyama, sisi tunafuata miongozo ya kuogelea na Papa Potwe. Boti za utalii na wavuvi wote wanafuata miongozo," alisema.


Kilopola amesema utafiti wa 2025 umethibitisha jambo la kipekee duniani.


"Papa Potwe ni spishi inayotembea sana (highly migratory). Lakini Mafia ndiyo sehemu pekee duniani ambapo Papa Potwe anaishi kwa muda mrefu. Zamani alisemekana anaonekana Oktoba hadi Februari, sasa unaweza kumuona Julai hadi Aprili kwa sababu ya mazingira salama," amesema Kilopola.


Kwa sasa, watalii zaidi ya 6,000 huja Mafia kila mwaka kwa ajili ya Papa Potwe pekee, wengi wakiwa watalii wa nje na Watanzania wachache.


"Nawakaribisha Watanzania na wageni wa nje, Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla waje Mafia kumuona Papa Potwe. Ni fahari ya Mafia, fahari ya Tanzania. Papa Potwe anafika hadi mita 18 duniani, lakini Mafia tuna vijana wa mita tatu hadi nane.

No comments:

Post a Comment